Martial aandika historia, Liverpool ikiweka ubingwa mlangoni

Muktasari:

  • Martial alijiunga na Manchester United mwaka 2015 akitokea Monaco kwa ada ya uhamisho kiasi cha Pauni 35 milioni

Manchester,England. Mshambuliaji wa Manchester United, jana aliandika historia ya kuwa mchezaji wa kwanza wa timu hiyo kufunga mabao matatu katika mchezo mmoja, ‘hat trick’ tangu aliyewahi kuwa kocha wa timu hiyo, Sir Alex Ferguson kuondoka mwaka 2013 baada ya kuiongoza United kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Sheffield United katika Uwanja wa Old Trafford.

Tangu Robin Van Persie alipofanya hivyo dhidi ya Aston Villa mwaka 2013 ambao ndio ulikuwa wa mwisho kwa Ferguson kuinoa timu hiyo, hakuna mchezaji mwingine wa United aliyeweza kufunga mabao matatu katika mchezo mmoja kama alivyofanya Martial jana.

Martial alipachika mabao hayo matatu yaliyoiwezesha United kufikisha pointi 49 na kunyemelea kwa ukaribu nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, aliyafunga katika dakika ya 7, 44 na 74.

Lakini wakati Martial akitamba upande wa United,  Liverpool imeusogelea karibu zaidi ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu huu baada ya jana kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 nyumbani dhidi ya Crystal Palace.

Trent Alexander-Arnold alianza kuifungia Liverpool katika dakika ya 23 na ikaongeza mabao mengine kupitia kwa Mohamed Salah, Fabinho na Sadio Mane katika dakika za 44, 55 na 69.

Ushindi huo umeifanya Liverpool ifikishe jumla ya pointi 86 ambazo zinaweza kuwafanya watangaze ubingwa leo ikiwa Manchester City wanaoshika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi na pointi zao 63, watafungwa au kutoka sare na Chelsea katika mechi watakayocheza leo usiku.

Baada ya mchezo huo kocha wa Liverpool Jurgen Klopp alifunguka na kueleza kuwa, wachezaji wake walicheza kwenye kiwango cha juu sana.

" Tumeonesha kiwango cha kupindukia, na kutoa kila tulicho nacho, jambo ambalo limetufanya leo kuwa kwenye nafasi hii tuliyopo" Alisema.

Katika mechi nyingine, Aston Villa anayochezea Mtanzania, Mbwana Samatta ilitoka sare ya bao 1-1 na Newcastle, Norwich walifungwa bao 1-0 na Everton na Wolves iliichapa Bournemouth kwa bao 1-0.

Ligi hiyo itaendelea tena leo ambapo jumla ya michezo minne itachezwa katika viwanja tofauti.

Hapana shaka, mechi baina ya Chelsea dhidi ya Manchester City ndio itakuwa mchezo utakaovuta hisia za wengi leo lakini kutakuwa na mchezo mwingine baina ya Southampton na Arsenal wakati Burnley wataikaribisha Watford.