Manji aongeza mzuka Yanga

Muktasari:

  • Yusuf Manji kwa mujibu wa TFF si Mwenyekiti wa Yanga, lakini wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wanaamini yeye ndiye na kutoa sababu zifuatazo. Kama Manji si Mwenyekiti kwa nini walimtoa madarakani aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga kwenye ubosi wa Bodi ya Ligi kwa madai hana sifa.

HUKO Jangwani unaambiwa mzuka umepanda kinoma, wakati Yanga ikirejea kwenye Ligi Kuu Bara kugawa dozi, huko klabuni wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wakimsubiri kwa hamu bilionea na mwenyekiti wao wa zamani, Yusuf Manji.

Wanachama na mashabiki hao wameaingalia kalenda na kubaini kuwa, leo ni Januari 15, tarehe ambayo bilionea huyo aliwaahidi kupitia barua yake iliyosomwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa klabu hiyo, George Mkuchika.

Mkuchika, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, alinukuu barua aliyoandikiwa na Manji kwamba angeanza shughuli zake rasmi Januari 15 ikiwamo kutinga klabu hapo.

Hata hivyo, bado wanachama na mashabiki hao wameendelea kusisitiza kuwa, wanaendelea kumsikilizia bilionea wao huyo wakiamini ataungana nao hata kwenye mchezo huo utakaopigwa saa 10:00 jioni.

Mpaka alasiri ya jana hakukuwa na taarifa zozote kama Manji angetinga Jangwani kama alivyoahidi, huku Mkuchika akisisitiza alichokisoma ndivyo alivyokuwa ameandikiwa na hana lingine alijualo kwa sasa ila watafutwe viongozi wa Yanga.

Hata hivyo, viongozi wa Yanga hawakupatikana kwa madai walikuwa wakishughulika na ishu ya kesi waliyofunguliwa na wanachama wao waliouzuia Uchaguzi Mdogo wa klabu hiyo uliokuwa ufanyike juzi Jumapili.

Kesi hiyo ilifunguliwa Ijumaa kwenye Mahakama ya Kisutu na kukwamisha uchaguzi huo ambao, ulikuwa ukimuondoa rasmi Manji kwenye nafasi ya Uenyekiti kwani, nafasi yake ilishapata wagombea wawili Mbaraka Igangula na Dk. Jonas Tiboroha.

Licha ya kutokuwepo kwa uhakika kama Manji ataonekana hadharani Yanga, mashabiki wa klabu hiyo wamekuwa na mzuka zaidi baada ya kubaini, chama lao leo litakuwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuvaana na Mwadui ya Shinyanga.

Waanamini huenda Manji akaibukia Taifa kuwahamisha vijana wake ili kuendeleza rekodi yao ya kupototeza mechi katika Ligi Kuu Bara na kuongeza pengo la pointi baina yao na watani zao wa Simba hadi kufikia 20 kwani, Msimbazi wameahirishwa tena mechi yao iliyokuwa ipigwe leo Jumanne mjini Iringa dhidi ya Lipuli FC.

Yanga ipo kileleni ikiwa na alama 50, ikifuatiwa na Azam FC itakayocheza kesho Jumatano na Ruvu Shooting ikiifuata na alama zao 40 na Simba ikiwa ya tatu na alama 33, baada ya kushuka uwanjani mara 14 tu, huku ligi ikiwa raundi ya 21. Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera aligoma kuelezea maandalizi ya mchezo huo na kutaka Msaidizi wake, Noel Mwandila azungumze, lakini naye aliamua kukausha akidai hajapewa ruksa na bosi wake.

Hata hivyo, ni kwamba Yanga itashuka uwanjani leo ikiwa na uhakika wa kuendelea kumtumia nahodha wake msaidizi, Andrew Vincent ‘Dante’ aliyekwepa rungu la adhabu ya kifungo kutoka Kamati ya Nidhamu ya TFF, japo itawakosa baadhi ya nyota wake muhimu akiwamo straika Heritier Makambo aliyetarajiwa kutua nchini usiku wa jana.

Nyota hao alikwenda kwao DR Congo kwenye matatizo ya kifamilia, lakini bado Yanga itawategemea wakali wengine akiwamo nahodha mpya, Ibrahim Ajibu kuendesha vitai dhidi ya Mwadui waliotamba wamekuja kuzoa pointi.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Mwadui, Ally Bizimungu alisema wanaingia wakiiheshimu Yanga, japo hawana hofu dhidi yao.

“Jambo la msingi ni wachezaji wangu kucheza kwa umakini wa hali ya juu na kutofanya makosa yanayoweza kuwapa nafasi wapinzani wetu kutuadhibu.

Yanga ni timu kubwa na itakuwa nyumbani lakini mwisho wa siku mpira unachezwa uwanjani,” alisema Bizimungu.

Katika hatua nyingine hatma ya uchaguzi wa Yanga imeshindwa kubainika kutokana na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Ally Mchungahela kutwa nzima ya jana kushindwa kutolea ufafanuzi kwa madai alikuwa bize akishughulikia ishu hiyo. Awali, Mchungahela alisema jana Jumatatu angetoa kauli juu ya hatma ya uchaguzi aliouahirisha kutokana madai ya kufunguliwa kesi kadhaa

Kesi hiyo ya Yanga imefunguliwa na wanachama Juma Magoma na Athuman Nyumba ikiwa ni ya kikatiba namba 1/2019 ikipinga uchaguzi huo wa Yanga kufanyika kinyume cha katiba yao.

Magoma na Nyumba walifungua shauri hilo Januari 11, 2019 na kupangwa kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega. Katika madai yao wakipinga kufanyika kwa uchaguzi huo kwa madai ya unakwenda kinyume na katiba ya Klabu ya Yanga ya mwaka 2010 ibara ya 7.

Ibara hiyo inaelezea utaratibu wa uanachama ndani ya Klabu ya Yanga ambao, kwanza ni kutuma maombi, ambapo maombi hayo yatapelekwa kwa Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga, ambaye baaade yatajadiliwa na kamati tendaji.

Pia, ibara hiyo, inaelezea kuwa maombi hayo yataambatana na fomu namba YASC/U, ada ya uanachama ambayo ni Sh 12,000 pamoja ana ada ya kadi ambayo ni Sh 2000. Hakimu Mtega aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 24, 2019, itakapotajwa.

Baadhi ya viongozi waliojiudhuru ndani ya klabu hiyo ni Yusuph Manji ambaye alikuwa mwenyekiti wa klabu ya Yanga, makamu wake Clement Sanga pamoja na wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji.

Wajumbe hao waliojiudhuru ni Hashimu Abdallah, Salum Mkemi, Omari Saidi na Ayub Nyenzi.