Mambo haya manne kuzibeba Simba, Yanga, Azam na KMC CAF

Muktasari:

  • Mara baada ya uamuzi huo wa CAF, Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana kwa dharura na kuteua timu za Simba iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Yanga iliyoshika nafasi ya pili kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika huku Azam FC iliyotwaa ubingwa wa Kombe la FA na KMC iliyomaliza nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu zikipewa nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika.

Dar es Salaam.Tanzania ina kila sababu ya kujivunia baada ya uamuzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuamua kuwa msimu ujao wa mashindano yake kwa ngazi ya klabu wa 2019/2020, Tanzania itawakilishwa na klabu nne.

Awali baada ya Tanzania kufikisha pointi 18 zinazoifanya iwe miongoni mwa nchi 12 ambazo kila moja inaingiza timu nne kwenye mashindano ya klabu Afrika, ilifahamika kuwa hilo litakuwa kwenye msimu wa 2020/2021 lakini Kamati ya Utendaji ya CAF iliyokutana huko Paris, Ufaransa iliamua hilo liwe kwa msimu ujao.

Mara baada ya uamuzi huo wa CAF, Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana kwa dharura na kuteua timu za Simba iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Yanga iliyoshika nafasi ya pili kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika huku Azam FC iliyotwaa ubingwa wa Kombe la FA na KMC iliyomaliza nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu zikipewa nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika.

Hata hivyo furaha ya kuwakilishwa na timu nne haitokuwa na maana ikiwa klabu hizo za tanzania zitashindwa kutamba kwenye mashindano hayo zitakazoshiriki na badala yake kuwa wasindikizaji.

Ni lazima timu hizo zifanye vizuri kwani mbali ya kuitangaza nchi lakini pia itasaidia kuzidi kuongeza idadi ya pointi za Tanzania katika viwango vya ubora vya CAF ambavyo hutumiwa katika kuamua idadi ya timu ambazo nchi husika inapeleka kwenye mashindano ya kimataifa.

Kufanya huko vizuri ni matokeo ya maandalizi maqzuri ambazo timu hizo zinapaswa kufanya kabla ya kuanza kwa mashindano hayo na kama ikiwa kinyume, hakuna cha maana ambacho Simba, Yanga, Azam na KMC zitavuna kwenye mashindano hayo.

Tathimini ya mambo ambayo yanaweza kuzibeba timu hizo kwenye mashindano ya kimataifa na pia changamoto zinazoweza kuziangusha kufanya vyema pindi kipyenga cha Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika kitakapopulizwa.

Usajili imara

Katika msimu uliomalizika, timu hizo zote nne zilikuwa na udhaifu kwenye baadhi ya maeneo ambao ni lazima uondolewe ili ziweze kutamba kimataifa na hilo linaweza kukamilika ikiwa zitafanya usajili wa wachezaji wazuri wa kucheza kwenye nafasi ambazo zinahitaji kuimarishwa.

Simba licha ya kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliomalizika, inatakiwa kusajili angalau wachezaji watano ambao ni beki wa kulia, beki wa kati mmoja, kiungo mmoja mkabaji, winga na mshambuliaji.

Yanga kama ilivyo kwa KMC na Azam nazo zinapaswa kusajili nyota wenye daraja la juu wasiopungua saba ili waweze kupambana na kuisaidia timu kwenye mashindano hayo.

nafasi ambazo timu hizo ni lazima ziongeze watu ni golini, beki wa kushoto, viungo wa kushambulia na ulinzi, mawinga, namba nane na washambuliaji wa kati.

Lakini pia zinapaswa kuhakikisha kila moja inabakiza nyota wake muhimu kikosini ambao walifanya vizuri msimu uliomalizika.

Bajeti ya Kutosha

Mpira ni pesa na huwezi kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa kama hauna bajeti ya kutosha kukuwezesha kusafirisha timu kutoka nchi moja kwenda nyingine, kugharamia huduma kama posho, kambi, mishahara, matibabu na programu za mazoezi pamoja na kugharamia masuala ya usajili na kuimarisha benchi la ufundi.

Inawezekana timu ikafanya vizuri bila kutumia kiasi kikubwa cha fedha kwenye bajeti yake lakini angalau bajeti hiyo inapaswa kukidhi mahitaji muhimu ya timu vinginevyo ni vigumu kuona mafanikio yakipatikana.

Benchi imara la ufundi

Kuna sababu kwa timu hizo nne kila moja ikatanua benchi lake la ufundi kwa kuongeza wataalam ambao watakuwa na jukumu la kumsaidia kocha mkuu kutimiza majukumu yake ya kiufundi.

Ni vigumu kwa timu kutamba kwenye mashindano ya kimataifa kama haina benchi pana kwa sababu uwepo wa idadi kubwa ya wataalamu kwenye benchi la ufundi inasaidia katika kuzisoma timu pinzani, kuwajenga wachezaji kimwili na kisaikolojia,

Faida ya kuwa na benchi pana la ufundi ilionekana kwa Simba ambayo uwepo wa mtaalam wa viungo kutoka Tunisia, Adel Zrane ambaye amesaidia timu hiyo kuwa na wachezaji walio fiti ambao waliweza kuhimili ushindani dhidi ya wachezaji wa timu bora kama Al Ahly, Nkana FC, TP Mazembe, AS Vita na Mbabane Swallows.

Maandalizi mazuri

Kabla ya msimu kuanza, ni vyema Simba, Azam, Yanga na KMC zikajipanga vyema kiufundi kwa kufanya maandalizi bora ya mwanzoni mwa msimu (pre season) nje ya nchi ili ziweze kutengeneza uelewano wa vikosi vyao kwa haraka lakini pia stamina, pumzi na ufiti wa wachezaji wao.

Ni jambo lililo wazi kuwa hapa nchini bado hakujawa na miundombinu na vifaa bora vya mazoezi kuweza kuifanya timu ipate maandalizi mazuri ya mwanzoni mwa msimu hivyo kambi za nje ya nchi zitasaidia kufanikisha hilo.