Makonda awasili Cairo ataka ushindi kwa Taifa Stars -VIDEO

Wednesday June 26 2019

 

Cairo, Misri. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewasili jijini Cairo asubuhi hii tayari kwa kuongeza hamasa kuelekea mchezo wa kesho wa Taifa Stars dhidi ya Kenya.

Makonda amepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Misri Meja Jenerali Mohamed Nassoro pamoja na Rais wa TFF, Wallece Karia.

Baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Cairo, Makonda alisema bado anaamini Stars inaweza kufanya vizuri katika mechi zake mbili zilizosalia.

Makonda alisema kwa sasa mara baada ya kuwasili anataka kwanza kuonana na wachezaji kujua hali zao kabla ta mechi ya kesho.

Kiongozi huyo alisema shabiki kweli na mzalendo hawezi kukata tamaa baada ya Stars kupoteza mechi ya kwanza.

Alisema Stars ina wachezaji bora ambao bado wana nafasi ya kufanya vyema mbele ya Kenya iliyopoteza mechi ya kwanza pia.

Advertisement

Makonda katika msafara wake ameungana na Hery Said ambaye ni katibu wa kamati ya hamasa ya Stars.

Mapema jana akizungumza katika ufunguzi wa Mradi wa Gesi, Kigamboni, Makonda alisema ameshangaa wadau mbalimbali wakiwazungumzia vibaya wachezaji baada ya kupoteza mbele ya Senegal.

"Nimeumizwa na matokeo ya Taifa Stars, lakini nimeumizwa zaidi kwa watu kuwabeza wachezaji wetu ambao wametubeba watanzania ambao ndani ya miaka 30, haikuwezekana lakini wao wamepambana mpaka tupo Afcon leo hii," alisema Makonda.

Advertisement