Majeruhi Namungo Wamtikisa Hitimana

LICHA ya kuanza na ushindi kwenye mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu Bara, Kocha Mkuu wa Namungo, Hitimana Thierry amekiri ligi ya msimu huu itakuwa na ushindani mkubwa, lakini kinachomtisha na hali ya majeruhi kuwepo kwenye kikosi chake mapema.

Hitimana aliyeiwezesha Namungo kufika fainali ya Kombe la ASFC na kumaliza nafasi ya nne kwenye msimu wa ligi uliopita na kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika, alianza na ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union na kumfanya achekelee kulipa kisasi dhidi ya wapinzani hao.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo alisema kuanza kwa ligi huku timu mbili tu zikipata ushinda zaidi ya bao moja, yaani Simba na KMC ni dalili kwamba msimu huu kazi itakuwa kubwa kuliko iliyopita, lakini kwake presha imeanza mapema kutokana na kuwa na majeruhi mapema.

Hitimana alisema ndani ya kikosi chache kwa sasa kuna wachezaji wanne muhimu ambao wote ni majeruhi, akiwamo Hashim Manyanya, Steven Duah, Edward Charles na Carlos Protus hali ambayo inamtibulia mipango aliyokuwa nayo awali, licha ya kukiri bado ana wachezaji wa kuziba nafasi zao kwa ufanisi.

“Edward (Charles Manyama) na Hashim Manyanya wameumia kifundo cha mguu, Carlos Protus ni majeruhi wa paja, Stephen Duah aliumia mguu katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba. Majeruhi hawa wananitia hofu, kwani ni watu ninaowategemea katika kikosi cha kwanza na mechi ijayo dhidi ya Polisi nitawakosa,” alisema kocha huyo raia wa Burundi.