MO Salah aanza mambo

Saturday August 10 2019

 

LIVERPOOL, England. MABINGWA wa Ulaya, Liverpool wameianza Ligi Kuu ya England kwa kishindo baada ya usiku wa kuamkia leo kuifumua Norwich City  iliyorejea kwenye ligi hiyo kwa mabao 4-1, huku straika wao mkali Mohamed Salah akianza hesabu kwa kutupia bao mojawapo.
Salah aliyemaliza kama Mfungaji Bora msimu uliopita akifungana Sadio Mane anayecheza wote Liverpool na Emerick Aubameyang wa Arsenal, alifunga bao lake la kwanza msimu huu dakika ya 19 likiwa bao la pili la Liverpool katika mchezo huo uliopigwa Anfield.
Beki wa wageni, Grant Hanley kujifunga dakika ya saba katika harakati za kuokoa krosi ya Divock Origi kabla ya Virgil van Dijk kufunga bao la tatu dakika ya 28 na Origi kuongeza la dakika ya 42 na kufanya hadi mapumziko Majogoo hao kuwa mbele kwa 4-0.
Norwich City ilirejea kipindi cha pili ikiwa na utulivu na kuwabana wenyeji wao sambamba na kutengeneza nafasi kadhaa na kubahatika kupata bao la kufutia machozi liliowekwa kimini na Teemu Pukki dakika ya 64.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea jioni ya leo kiwa michezo kadhaa ukiwamo ya mapema mchana huu, West Ham United itakapoikaribisha watetezi wa EPL, Man City na kesho mashabiki watakuwa na hamu ya mchezo kati ya Manchester United na Chelsea.

Advertisement