Liverpool wakijipindua tu wanapigwa chini Ulaya

Muktasari:

Barcelona wao wamekusanya pointi 11 kwenye mechi zao tano walizocheza katika Kundi F. Chelsea nao wanasubiri hadi mchezo wa mwisho watakapocheza na Lille kutambua hatima yao baada ya sare ya 2-2 kutoka kwa Valencia kuwafanya kufikisha pointi nane sawa na Valencia.

LIVERPOOL, ENGLAND . MABINGWA watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Liverpool wamejiweka kwenye hatari ya kushindwa kutinga hatua ya mtoano ya 16 bora kama hawatashinda na kukumbana na kipigo kwenye mchezo wa mwisho wa Kundi E.

Liverpool kwenye mechi tano ilizocheza hadi sasa imevuna pointi 10, moja tu zaidi ya Napoli baada ya sare yao ya 1-1 uwanjani Anfield, juzi Jumatano. Mchezo wa mwisho wa kikosi hicho cha Jurgen Klopp watakabiliwa kwenye kucheza ugenini kwa RB Salzburg, ambao kwa sasa wa pointi saba baada ya juzi kuichapa Genk ya Ubelgiji 4-1.

Kwenye kundi hilo, Liverpool wana +3 ya tofauti yao ya mabao ya kufunga na kufungwa, wakati Salzburg wao wana +5 kwenye tofauti ya mabao yao ya kufunga na kufungwa, hivyo Liverpool wakipoteza mechi hiyo ya mwisho kisha Napoli wakashinda au kutoka sare tu na Genk basi watakuwa wamewasukuma nje mabingwa hao watetezi na kwamba watahamia kwenye Europa League.

Kwa maana hiyo, mechi ya RB Salzburg ni kufa kipona kwa Liverpool. Katika mechi zilizochezwa juzi, Barcelona ndio waliofanikiwa kutinga hatua ya mtoano baada ya ushindi wao wa mabao 3-1 dhidi ya Borussia Dortmund na kuwaachia shughuli ya kutafuta nafasi ya pili, Inter Milan na Dortmund, ambao kila mmoja amekusanya pointi saba.

Barcelona wao wamekusanya pointi 11 kwenye mechi zao tano walizocheza katika Kundi F. Chelsea nao wanasubiri hadi mchezo wa mwisho watakapocheza na Lille kutambua hatima yao baada ya sare ya 2-2 kutoka kwa Valencia kuwafanya kufikisha pointi nane sawa na Valencia.

Ajax wao wana pointi 10 na watamaliza mechi ya mwisho na Valencia. Matumaini kwa kocha Frank Lampard ni kwamba mchezo wa mwisho utapigwa Stamford Bridge dhidi ya Lille, ambao wao wamekusanya pointi moja tu katika Kundi H.