Lipuli yampa akili Makatta

Friday August 23 2019

 

By Matereka Jallu,Dodoma

USHINDI wa bao 1-0 iliyopata Dodoma Mji FC mbele ya Lipuli Iringa wala haijamvimbisha kichwa Kocha Mbwana Makatta, badala yake umezidi kumpa akili katika mbinu za kuipandisha Ligi Kuu timu yake iliyopo Daraja la Kwanza (FDL).

Dodoma ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kwa bao la Anwar Jabir aliyemtungua kipa Aghaton Anthony kwa shuti la mguu wa kushoto, licha ya kucheza muda mrefu ikiwa pungufu kutokana na Rajabu Mgalula kupewa kadi nyekundu kwa kumtolea lugha chafu Mwamuzi, Florentina Zablon katika dakika ya 35.

Licha ya Lipuli iliyopo Ligi Kuu Bara na kutinga fainali ya Kombe la FA kwa msimu uliopita kucharuka kusaka bao la kusawazisha, ilipoteza penalti katika kipindi cha pili kupitia kwa Jimmy Shoji aliyepiga mkwaju uliopanguliwa na kipa, Dotto Masalanga Wanapaluhengo walitoka vichwa chini, huku Kocha wa Dodoma, Makatta akifunguka.

Kocha huyo aliyezipandisha Ligi Kuu, Aliance na Polisi Tanzania kwa vipindi tofauti alisema ushindi huo, umechangia kumpa sababu ya kufikia malengo ya kuivusha hadi Ligi Kuu timu hiyo na katu habweteki.

“Kucheza mechi ngumu dhidi ya timu kama Mbeya City na Lipuli kumetuimarisha mno na tumepata matokeo kwenye mechi zote mbili huku tukitengeneza nafasi nzuri, hiyo inatupa sababu za kuamini tutafanikisha lengo letu tulilojiwekea,” alisema Makatta.

Alisema anayachukua matokeo ya mechi zote kama chachu ya kuzidi kuimarisha kikosi chake kabla ya kuanza kwa FDL mwezi ujao ili arejee alichokifanya akiwa Alliance ya Mwanza na Polisi Tanzania ambazo zote zilimtema baada ya kuzipandisha hadi Ligi Kuu ya Tanzania.

Advertisement

Naye Kocha wa Lipuli, Haruna Harerimana alisema wachezaji wake walicheza kwa uoga kuhofia kuumia wakati wanaelekea kwenye ligi ila amepata kipimo kizuri kwenye mchezo huo na atayafanyia kazi mapungufu aliyoyaona ili wafanye vema kwenye mechi za Ligi Kuu Bara inayoanza kesho Jumamosi, huku timu hiyo ikitarajiwa kufungua pazia dhidi ya Mtibwa Sugar Jumapili kwenye Uwanja wa Samora, mjini Iringa.

Advertisement