Kwa hili la Morrison, Molinga awe mfano wenu

Muktasari:

Naamini lile la Molinga litakuwa limetufunza kitu twendeni tukapambane (dhidi ya Simba) kwa ajili ya timu yetu.

HABARI zenu mashabiki wangu wa Yanga. Ni imani yangu kuwa mko salama mkiendelea na majukumu ya kujipatia kipato kila mmoja na kazi yake huko mliko. Unajua maisha bila kupambana ni kazi bure. Ni sawa na kuendesha baiskeli pale unapoacha kukanyaga pedeli kila kitu nacho kinasimama.

Binafsi naendelea vyema nipo kwenye mazoezi nikisubiri ruhusa ya madaktari na makocha kuangalia ni jinsi gani nitarejea kwenye majukumu. Soka ni kazi yangu ukweli ni kwamba natamani kurudi uwanjani, nimewakumbuka mashabiki wangu na hata wale wa timu yangu.

Najua kila shabiki wa soka anawaza juu ya Julai 12, 2020 pale Yanga tutakapokutana na Simba, punguzeni presha kila kitu kitakuwa sawa kwani Yanga tuna malengo na wao (Simba) wana malengo yao. Acha tukapambane uwanjani.

Najua Simba ni timu nzuri, lakini Yanga tuna ubora na malengo yetu hivyo acha kila timu ikajiandae tukutane uwanjani wala msiogope sana njooni mtupe nguvu uwanjani nyie ni watu muhimu kwetu.

Leo nitakuwa na muda wa kuongea nanyi kuelekea mechi hii dhidi ya Simba kuna jambo muhimu nataka nishauriane nanyi mashabiki wa klabu yetu pendwa. Kuna wakati fulani ndani ya klabu yetu uliopita upepo mbaya juu ya washambuliaji wetu hasa David Molinga na Yikpe Gnamien ambao hawakuwa na upepo mzuri katika ufanisi wa kazi yao.

Upepo ule uliwasababishia hali ambayo haikuwa nzuri kwa mashabiki wa klabu yetu waliokuwa wakali kuliko maelezo hawakutaka kuelewa kwanini timu haifungi.

Ukiangalia mashabiki walikuwa sahihi kuhuzunika na hali ile lakini naona wakienda mbali zaidi kwa kuwa wakali kwa wachezaji wao lakini binafsi nilikuwa na mtazamo tofauti juu ya hali ile.

Namjua Molinga sikukutana naye hapa Tanzania ni Mkongomani mwenzangu na ameshafanya kazi bora sehemu mbalimbali alikocheza tena kwenye ligi ngumu kuliko hapa niliamini kwamba ni upepo mbaya tu ulikuwa unampitia kwenye timu.

Imani yangu pia ilitokana na wakati anashambuliwa alikuwa ndio mfungaji bora kwenye timu yetu ya Yanga.

Baadaye mambo yalikaa sawa na Molinga akaanza kufunga, nilifurahi kuona mashabiki waliokuwa wanamzomea wakimuomba radhi kwa ile hatua yao ya awali, hili lilipendeza kudumisha uungwana.

Pia imani yangu hiyo inakwenda kwa Yikpe kama akiaminiwa anaweza kufanya vizuri na kuja kuisaidia klabu hata katika mechi hii muhimu ni kuendelea kumuamini kwa kuwa ndio wachezaji tulionao.

Jumapili timu itakuwa uwanjani na tunakutana na Simba, lakini hapa kati kuna vurugu ziliendelea juu ya rafiki yangu Bernard Morrison. Baada ya sakata la muda sasa Morrison amerejea kwenye timu yapo ambayo nimeongea naye kama kiongozi wake na kuna mambo ameniahidi kuwa atayafanya uwanjani siku hiyo.

Mashabiki wa timu yangu nitumie nafasi hii kuwaomba kuwa watambue Morrison alikuwa na tofauti na uongozi wa klabu yetu na kurejea kwake kuna maana kwamba kuna utulivu wa maelewano umefanyika na viongozi kuridhia na kati yetu sisi hakuna anayejua kwa undani nani alikosea vipi kwa mwenzake kati ya uongozi na Morrison.

Hili hatupaswi kuliingilia sisi zaidi ya kumpokea mtoto aliyetaka kutoka nyumbani ambaye ameamua kurejea ndani kuungana na familia yake. Nitafurahi kuona mashabiki wa timu yetu wakimpokea kwa furaha kijana wao ambaye amerejea kwa ari kuwatumikia ikiwezekana watambe kuwa mtoto wao amerejea na kumpa nguvu ili aitumikie familia nafikiri hili litasaidia kumpa elimu Morrison juu ya maisha anayotakiwa kuishi ndani ya Yanga.

Hata sisi kama wachezaji tumeamua kumwelewa Morrison baada ya kuzungumza nasi mara baada ya kurejea na hatua hii tumeamua kuwaachia wao Morrison na uongozi wamalizane muhimu ni kuitumikia Yanga.

Ninachofahamu kuhusu mashabiki wa Yanga ni waungwana sana lakini pia ni waungwana kwa mchezaji muungwana sina wasiwasi kwamba kama Morrison atafanya kazi yake vizuri kuna uwezekano mkubwa mashabiki wa Yanga nao watafurahia kazi yake kulingana na aliyoniahidi kama nahodha wake.

Yanga ina malengo yake katika mechi hii muhimu ni vyema mashabiki, viongozi na wachezaji wakaungana kuhakikisha tunafanikiwa katika vita hii ngumu na sio kuanza kutoana dosari, hayo yafanyike baada ya mchezo tukiwa tumetulia. Kama ikitokea Morrison akapokewa vibaya hali hiyo inaweza kumuondoa mchezoni na kujikuta tunaharibu utulivu wa timu mapema, naamini lile la Molinga litakuwa limetufunza kitu twendeni tukapambane kwa ajili ya timu yetu.