Kumbe Manji bado akumbukwa buana

Muktasari:

  • Jimmy anakumbukwa kwa kituko alichokifanya kwenye mchezo wa mzunguko wa pili wa watani wa jadi kati ya Simba na Yanga kwa kumbetia mke wake ambaye hata hivyo alirejeshewa baada ya timu yake kupoteza kwa bao 1-0.


SI mnamkumbuka yule shabiki wa Yanga, Jimmy Kindoki aliyebetia mke siku ya pambano la watani wa jadi nchini? Jamaa buana amesema ni vigumu kwa Wanayanga kumsahau aliyekuwa mwenyekiti wao, Yusuf Manji kwa makubwa aliyokuwa akifanya kwenye klabu hiyo.

Jimmy alisema hilo kutokana na kuangalia kwake aina ya wagombea waliochukua fomu na majina yao kupitishwa kwenye usahili uliofanywa siku chache zilizopita.

Shabiki huyo aliyejizolea umaarufu mkubwa Yanga, alisema kiongozi atakayechukua nafasi hiyo atakuwa na mtihani mkubwa wa kuwasahaulisha wadau na mashabiki wa Yanga kuhusu Manji kiutendaji.

“Manji alikuwa zaidi ya kiongozi, aliweza kutumia fedha zake kama mwenyekiti kutatua changamoto mbalimbali za klabu, tuliweza kwenda kuweka kambi Uturuki ni kwa ajili ya uwepo wake.

“Yanga hapakuwa na matatizo ya wachezaji kutopata mishahara yao kwa miezi zaidi ya mitatu, hatuna neno naye atabaki kuwa mmoja kati yetu ni kipenzi cha wanayanga.

“Tunaweza kumbuka Manji zaidi endapo atakayeingia akiwa mbabaishaji, naomba Mungu atusaidie kupata kiongozi sahihi atakayeweza kurejesha zama zile ambazo tulikuwa tukitesa, “ alisema shabiki huyo.

Wagombea waliopitishwa kwenye usahili katika nafasi ya mwenyekiti ni Dkt Mbette Mshindo Msolla na Elias Mwanjala.

Jimmy anakumbukwa kwa kituko alichokifanya kwenye mchezo wa mzunguko wa pili wa watani wa jadi kati ya Simba na Yanga kwa kumbetia mke wake ambaye hata hivyo alirejeshewa baada ya timu yake kupoteza kwa bao 1-0.

Kurejeshewa mke wake kulitokana na kilio alichoangua baada ya Meddie Kagere kuifunga Yanga bao pekee lililowapa Simba alama tatu kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.