Kisa Ligi ya Mabingwa yampasua kichwa kigogo Simba SC

Muktasari:

Mazingisa alisema kuondolewa kimataifa kumeifanya timu hiyo kushindwa kujitangaza nje ya nchi na kupata fursa nyingi tu.

KITENDO cha Simba kuondolewa mapema kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na UD Songo ya Msumbiji, kimemvuruga mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Senzo Mazingisa ambaye amefafanua kutailazimu klabu hiyo kufanya marekebisho kadhaa ili iwe tishio zaidi na isirudie makosa siku za usoni.

Mazingisa alizungumza hayo katika mahojiano maalumu na gazeti hili hivi karibuni

“Ni zaidi ya huzuni ya kuondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, bodi imefanya kazi nzuri ya kubaki na maofisa wa benchi la ufundi lakini kutakuwa na badiliko moja au mawili lakini jambo la kufanya ni kuimarisha zaidi benchi la ufundi kwa ajili ya ubora wa timu.

“Tangu nimefika hapa nimekuwa nikifuatilia kila kitu kwa ukaribu. Na pendekezo la kocha lazima lifanyiwe kazi lakini tunatakiwa kutafuta suluhisho la kuimarisha zaidi timu,” alisema mtendaji huyo.

Ikumbukwe hadi sasa, Simba ndio klabu yenye benchi pana la ufundi hapa nchini kuliko lingine ambapo lina maofisa tisa.

Mazingisa alisema kuondolewa kimataifa kumeifanya timu hiyo kushindwa kujitangaza nje ya nchi na kupata fursa nyingi tu.

“Kucheza michezo ya kimataifa ni jambo zuri na lenye tija kwa timu. Hivyo tutajipanga vizuri kuhakisha makosa yaliyotokea hayajirudii tena,” alisema.

Kimataifa

Mazingisa alisema imefika wakati kwa Simba kunufaika kupitia fursa zinazoweza kupatikana kutokana na uhusiano wa klabu na taasisi nyingine za soka nje ya Tanzania.

“Nina kituo cha soka lakini pamoja na hilo, Simba inatakiwa kujenga ushirika sio tu na Afrika Kusini, bali pia programu nyingine zenye faida barani Afrika na kwingineko,” alisisitiza Mazingisa.

Alivyotua Simba

Mazingisa alisema hakuajiriwa na Simba kwa bahati mbaya, bali lilikuwa ni kutimia kwa ndoto zake za kufanya kazi nje ya Afrika ya Kusini.

“Nafasi ya mtendaji mkuu ilitangazwa na kwangu ilikuja katika muda mwafaka kwa sababu nilikuwa naangalia fursa nyingine, hivyo nikaamua kuiomba. Haikuwa Tanzania moja kwa moja, bali yalikuwa ni matarajio yangu kufanya kazi nje ya Afrika Kusini. Nilikuwa na hamu ya kujifunza, mpira unaendeshwaje katika nchi nyingine. Baada ya kufanya kazi kwenye soka kwa kipindi kirefu na kusafiri katika nchi tofauti, nilitaka kupata uzoefu zaidi. Kabla ya kuomba nafasi hii nilikuwa naijua Simba lakini pia hata Yanga. Pia, nazijua timu kubwa katika nchi nyingine za Afrika.

Mabadiliko simba

Kigogo huyo wa Simba alisema malengo hayo ya muda mfupi ya kuifanya Simba iwe taasisi inayoendeshwa kwa kufuata taratibu itakuwa chachu ya mafanikio kwa mipango ya muda mrefu ambayo ni kuifanya iwe klabu kubwa barani Afrika siku za usoni.

“Kubwa ni kuhakikisha ndani ya miaka michache ijayo, klabu inakuwa na uwezo wa kujitegemea yenyewe kwa kutengeneza vyanzo vyake vya mapato badala ya kutegemea udhamini.

Pia, ubunifu wa mawazo yanayoendana na muktadha wa soka la Afrika ili iwe miongoni mwa klabu bora barani Afrika.

Na moja ya vipaumbele ambavyo tunatakiwa kuvifanyia kazi ni kuwabadili mashabiki wetu kuwa wateja wetu kwa kutumia mtaji wa mashabiki ambao tayari tunao,” alisisitiza Mazingisa.

“Unapoboresha benchi la ufundi, pia unaweza kujenga timu na kukibadili kikosi kuwa na makali ndani uwanj,” alisema.

Nidhamu

Simba imetangaza hali ya hatari kwa wachezaji, maofisa wa benchi la ufundi pamoja na wafanyakazi wake kwa kupanga kutoa adhabu kali kwa yeyote atakayejihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu.Hivi karibuni wachezaji wanne wa timu hiyo, Jonas Mkude, Clatous Chama, Erasto Nyoni na Gadiel Michael walituhumiwa kujihusisha na vitendo hivyo.

Wachezaji hao hawakwenda Kanda ya Ziwa kwa mechi mbili za Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar na Biashara United pasipo ruhusa kutoka kwa uongozi huku Chama na Mkude wakiwa na kosa lingine la kutoroka kambini. Mazingisa aliliambia gazeti hili kuwa uongozi wa Simba hauungi mkono vitendo vilivyofanywa na wachezaji hao na utatoa adhabu kali kwa wahusika ambayo pia itakuwa endelevu kwa wengine, maofisa wa benchi la ufundi hadi watumishi wa klabu hiyo.

“Nitashughulikia ipasavyo vitendo vyote vya utovu wa nidhamu ambavyo vitafanywa na wachezaji, maofisa wa benchi la ufundi na maofisa wengine wa sekretarieti.

Hatua kali na stahiki zitachukuliwa na zaidi tutazitangaza kupitia vyombo vya habari,” alisema Mazingisa. Alisema anataka kila mmoja ndani ya klabu anawajibika kutimiza malengo.

“Mipango yangu ya muda mfupi ni klabu inakuwa na mfumo bora wa kitaasisi, kufanyia kazi maazimio ya bodi ya klabu lakini pia kusimamia suala la utawala,” alisema.