Ni Senzo Mazingiza ; Ile Simba next level ndo hii

Muktasari:

Lakini ni nani huyo Mazingiza, ambaye anakuja kushika wadhifa huo mkubwa wa kusimamia shughuli za kila siku za uendeshaji wa klabu hiyo?

Simba imepata mtendaji mkuu mpya wa klabu hiyo ambaye ni Senzo Mazingiza, raia wa Afrika Kusini atakayerithi nafasi inayoachwa na Crescentius Magori.

Hii ni mara ya kwanza kwa klabu hiyo kuwa chini ya mtendaji mkuu ambaye ni raia wa kigeni na pengine hata kwenye timu nyingine hilo halijawahi kutokea.

Mazingiza ana uzoefu mkubwa katika uendeshaji na usimamizi wa mchezo wa soka na ni wazi kwamba, kama Simba itamtumia vizuri, ataifanyia mambo makubwa siku za usoni.

Lakini ni nani huyo Mazingiza, ambaye anakuja kushika wadhifa huo mkubwa wa kusimamia shughuli za kila siku za uendeshaji wa klabu hiyo?

Elimu na ujuzi

Mazingiza ni msomi mbobezi wa masuala ya biashara na utawala akiwa na elimu ya juu aliyoipata Chuo Kikuu cha Wits Business School kati ya 2012 hadi 2013.

Alipata shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Vaal University of Technology alikosoma kuanzia 1998 hadi 2000 na elimu ya juu alipata katika shule ya General Smuts.

Ni mjuzi katika masuala ya ukocha, masoko, utawala wa michezo, utafiti, mitandao ya kijamii, biashara, uhusiano wa kijamii, udhamini na mipango, huduma kwa wateja na uongozi.

Lugha nne kichwani

Mazingiza anazungumza na kuandika kwa ufasaha lugha nne ambazo ni Kiingereza, Afrikaans, Kizulu na Kisotho.

Uzoefu uliopitiliza

Haijawa bahati mbaya au uamuzi wa kubahatisha kwa Simba kumpa nafasi Mazingiza kuwa mtendaji mkuu wa klabu hiyo.

Kwa kipindi cha takribani miaka 20 amehudumu kwenye soka na kupata uzoefu wa hali ya juu ambao kama Simba itamtumia vyema itanufaika na kupiga hatua kubwa.

Jina la Mazingiza lilianza kuingia rasmi kwenye uongozi wa soka mwaka 2001 alipoteuliwa kuwa meneja mkuu wa klabu ya Chuo Kikuu cha Pretoria, nafasi aliyoitumikia kwa miaka mitatu hadi 2004 alipoondoka na kujiunga na Bay United FC kutumikia nafasi ya mkurugenzi mtendaji.

Hapo alikaa kwa miaka minne na mwaka 2009, aliteuliwa kuwa kaimu mratibu wa mashindano ya Kombe la Dunia ambayo yalifanyika Afrika Kusini 2010, na aliitumikia nafasi hiyo kwa mwaka mmoja na miezi minane.

Kazi nzuri aliyoifanya kwenye fainali hizo ilimpa dili la kuteuliwa kuwa meneja mipango wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL), aliyoitumikia kuanzia 2010 hadi 2012.

Wakati akiitumikia Ligi Kuu ya Afrika Kusini, mwaka 2011 Orlando Pirates ilimwajiri katika nafasi ya meneja utawala na baadaye 2013 akajiunga na Platinum Stars aliyoitumikia hadi mwaka 2017 alipoamua kung’atuka akiwa meneja mkuu.

Baada ya kuondoka aliamua kujiunga na Kampuni ya Menza Group (PTY) aliyoitumikia kwenye nafasi ya mtendaji mkuu hadi anapojiunga na Simba.

Tuzo binafsi

Ni mshindi wa tuzo ya mtawala bora wa mwaka iliyotolewa na Idara ya Michezo ya Gauteng mwaka 2012.

Mkali wa Mataji

Mazingiza ni miongoni mwa watu wenye nyota ya mafanikio hasa katika kubeba mataji na ushahidi wa hilo unajionyesha katika nyakati alizotumikia Orlando Pirates na Platinum Stars.

Katika kipindi cha mwaka mmoja na miezi 10 aliyotumikia Pirates kama meneja utawala, timu hiyo ilitwaa mataji matatu ambayo ni Ligi Kuu ya Afrika Kusini mwaka 2012, Telkom Cup (2011) na MTN Super 8 mwaka 2011.

Aliachana na Orlando Pirates mwezi Juni 2013 akiwa ameiongoza kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ikumbukwe kwamba mwaka huo, timu hiyo nusura itwae ubingwa wa mashindano hayo lakini ikaangukia pua mbele ya Al Ahly kwenye hatua ya fainali na kumaliza ikiwa nafasi ya pili.

Lakini pia nyota ya mataji iliendelea kung’aa kwa Mazingiza kwani pamoja na udogo wa Platinum Stars ambayo alienda kuitumikia baada ya kutoka Pirates, timu hiyo ilitwaa mataji mawili ndani ya miaka minne aliyohudumu kwenye nafasi ya meneja mkuu.

Sekretarieti yake

Wakati ikimnasa Mazingiza, Simba pia inaendelea kusuka sekretarieti yake ambayo itasimamiwa na bosi huyo mpya na hadi kufikia jana, tayari ilishapata watumishi wanne watakaokuwa chini ya Mazingiza. Hao ni Gift Macha, ambaye amepata kufanya kazi na gazeti la Mwanaspoti kabla ya kujiunga na Azam Tv, atakayekuwa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano na Rabi Hume atasimamia kitengo hicho upande wa digitali.

Hashim Mbaga atakuwa bosi wa cheo kipya cha meneja wanachama huku Rehema Lucas akiwa ni meneja ofisi wa klabu hiyo.