Bosi mpya Simba atangazwa, Magori aaga -VIDEO

Muktasari:

Afisa Mtendaji mpya wa Klabu ya Simba, Senzo Mazingisa ametambulishwa leo Jumamosi kuchukua nafasi ya Clecsentius Magori.

KLABU ya Simba imemtambulisha rasmi Afisa Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa   kutoka Afrika Kusini anayeingia kuchukua majukumu yaliyoachwa na Crecsentius Magori ambaye ameaga rasmi.


Bosi huyo ametambulishwa rasmi leo Jumamosi kwenye mkutanano wa waandishi wa habari uliofanyika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.


Akitolea ufafanuzi mchakato wa kumpata kiongozi huyo, Magori alisema, nafasi iliombwa na watu wanane kati ya hao sita walikuwa Watanzania na wawili kutoka mataifa mengine ambapo mmoja ni Mmarekani na mwingine Afrika Kusini ambaye ni Mazingisa.


Magori alisema, pamoja na idadi ya watu hao kujitokeza achana na elimu, kigezo kikubwa walichokiangalia ni uzoefu na uongozi wao katika michezo.


"Uzoefu kwenye uongozi unaweza kuiongoza wizara au mambo mengine lakini si kwenye michezo. Hivyo, mbali na elimu, tulizingatia zaidi uzoefu wa mtu huyo kwenye michezo, tukaona Senzo ni mtu sahihi tuliyemtaka,"alisema Magori.


Alisema, kiongozi huyo alishapatikana muda mrefu lakini walichelewa kumtangaza kwa sababu hakuwa na kibali na kazi na sasa wanamtafutia kile cha makazi hivyo wakaona ni wakati sahihi wa kumtambulisha.


Akimwelezea Senzo, kiongozi huyo alisema, aliwahi kufanya kazi na klabu kama Orlando Pirates na Platnumz Stars zote za Afrika Kusini.


Magori alimaliza kwa kuomba radhi watu mbalimbali katika uongozi wake na sasa anakwenda kuwa mshabiki wa kawaida;

"Katika uongozi wangu kwenye kazi, nilitofautiana na watu wengi lakini sasa nakwenda kuwa kuwa shabiki wa kawaida naomba msamaha."