Kinyozi wa mastaa wa England anachaji Sh270,000 kwa kichwa

Saturday May 23 2020

 

LONDON ENGLAND. UMEWAHI kufurahishwa au kuchukizwa na mitindo ya nywele za mastaa wa Ligi Kuu England?

Unasemaje kuhusu mitindo ya nywele ya mastaa kama Wilfried Zaha na Mario Balotelli? Lakini, jambo kubwa umeshawahi kujiuliza ni nani, ambaye amekuwa akihusika na mitindo hiyo?

Maswali mengi yanayohitaji majibu. Kinyozi wao anaitwa, Nikky Okyere, mtu ambaye amekuwa bize kusakwa na mastaa hao wa Ligi Kuu England huku na kule kwa ajili ya kwenda kuwanyoa tu mitindo wanayotaka.

Kinyozi huyo mzaliwa wa Ghana, ndiye anayewanyoa mara nyingi, Zaha, Danny Welbeck, Jordon Ibe na mastaa wengine wa Ligi Kuu England. Hivi karibuni, amemsababishia matatizo makubwa staa wa Bournemouth baada ya kwenda kumnyoa, wakati wa kipindi cha kutakiwa kujifungia ndani na mbaya zaidi, video inayoonyeshwa akimnyoa imepostiwa kwenye Instagram.

Kinyozi, Nikky, 36, aliyetokea kwenye Jiji la Accra, amefungua saluni yake Kusini mwa London inayoitwa Slick Rick.

Kabla ya mastaa wa soka kutakiwa kujifungia ndani kufuatia mlipuko wa janga la virusi vya corona, Nikky alifanyiwa mahojiano kwenye saluni yake na kuelezea namna alivyopata umaarufu kwa kuwanyoa mastaa wa Ligi Kuu England na kuvuna mkwanja mrefu.

Advertisement

Kinyozi hiyo alisema kwamba aliwahi kupewa Euro 2,000 baada ya kwenda kumnyoa Balotelli, wakati alipotimiza umri wake wa miaka 25.

Alivyoanza ukinyozi

Nikky alisema kwamba alianza kumnyoa mtu akiwa na umri wa miaka 12, ambapo rafiki yake mmoja alitoka saluni, mahali ambako alinyolewa hovyo na hivyo yeye alilazimika kumrekebisha.

“Nikiwa Ghana, nakumbuka rafiki yangu mmoja alikwenda saluni kunyoa. Kipindi kile kulikuwa hakuna pesa. Wazazi wetu walikuwa wakitunyoa wenyewe, hivyo kwenda saluni ilikuwa ishu kubwa. Rafiki yangu huyo alipotoka saluni, hakuwa amenyolewa vizuri, hivyo nikalazimika kumrekebisha. Sikuwa nimewahi kumnyoa mtu kabla ya hapo, nilikuwa na umri wa miaka 12 tu. Nilimrekebisha kwa kitana na wembe tu, kwa sababu hatukuwa na uwezo wa kuwa na mashine ya kunyolea. Nilipomrekebisha, nilijigundua kwamba nina kipaji cha kuwa kinyozi. Baada ya hapo, marafiki zangu wote wakaanza kutaka niwanyoe. Hapo ndipo nilipoanza kuwa kinyozi.”

Mchezaji wa kwanza

Nikky alihamia London na kufungua saluni Camberwell na mchezaji wa kwanza kumnyoa alikuwa straika wa Portsmouth, Yakubu.

Baada ya hapo walifuatia wachezaji wengi mastaa kwenye Ligi Kuu England akiwamo Mghana mwenzake, kiungo Michael Essien.

“Kwanza nilikuwa kinyozi wa rafiki yake Yakubu. Kuna siku aliniambia hapendi staili ya nywele ya Yakubu, hivyo atamleta kwangu nimnyoe. Hivyo, alikuwa mchezaji wa kwanza kumnyoa, kitu ambacho kilikuwa heshima kubwa,” alisen Nikky.

“Sikuwa mtu wa kuweweseka na mastaa, kwa sababu mimi sikujali, ninachokipenda ni kukata nywele tu.

“Yakubu alinifanya nijiamini zaidi na sasa wala sina presha kwenye kukutana na mastaa wa Ligi Kuu England. Jamii inaona wanasoka ni mastaa wakubwa sana wasioingilika kirahisi, lakini Yakuku alikuwa akimsalimia kila mtu, alishikana mikono na kila mtu. Aliketi hapa kwenye kiti nimnyoe na akaanza kupiga stori za mambo mbalimbali, alikuwa mtu safi sana.”

Baada ya kunyoa staa huyo wa zamani wa Portsmouth, mastaa wengine wa Ligi Kuu England wakaanza kumimika kwenye saluni yake kunyolewa, hasa wachezaji weusi. Baada ya hapo, Mamadou Sakho, Bakary Sako, Jordon Ibe na Ahmed Musa wakamwalika Nikky aende kuwanyoa.

Wilfried Zaha

Staa wa Crystal Palace, Zaha ndiye aliyekuwa mchezaji wa kwanza kumtaka aende akamnyoe nyumbani kwake.

“Wilfried ndiye alikuwa mwanasoka wa kwanza kunialika nikamnyoa nyumbani kwake,” alisema Nikky.

“Kipindi kile alikuwa kwa mkopo Cardiff na aliponialika, nilifurahi sana. Alinitumia ujumbe kwenye mitandao ya kijamii kwamba anataka nikamnyoe. Aliniambia nikamnyoe, nilifurahi sana. Zaha ni kama mdogo wangu, hivyo nampenda kumweka vizuri nywele zake kabla ya mechi.”

Baada ya kuwa na uhusiano mzuri huo, jambo hilo lilimfanya Nikky kupata dili za kwenda kuwanyoa mastaa wengi wa Ligi Kuu England kwao akiwamo aliyekuwa staa wa Leicester City, Ahmed Musa. Nikky alisema wachezaji wengi kwenye Ligi Kuu England wanapenda kuonekana kwenye mwonekano mzuri kwa sababu ligi hiyo inatazamwa na mamilioni ya watu kupitia televisheni duniani kote na hivyo wamekuwa wakinyoa karibu kila wiki.

Gharama zake

Kwa mteja tu wa kawaida, anayetaka kunyoa na kwenda kwenye saluni yake, Nikky anamnyoa kwa Pauni 10, lakini kwa yule anayefanya booking na kwenda hapo saluni ni Pauni 20. Nikky alisema kwa wachezaji wanaompigia simu na kutaka akawanyoa wakiwa nyumbani kwao, amekuwa wakiwachaji Pauni 100, ambayo ni zaidi ya Sh 270,000 za Kitanzania.

Mfano mchezaji mmoja ambaye alimpigia simu na kutaka amkanyoa kwake ni Patrick van Aanholt, ambaye alimchaji Pauni 100.

“Kwa kawaida, nachaji Pauni 100, kwa mchezaji anayetaka nikamnyoe nyumbani kwake. Lakini, wachezaji wakati mwingine wamekuwa wakinipa pesa zaidi ya hiyo. Kuna wakati nilipata Euro 2,000 nilipokwenda kumnyoa Balotteli kwenye siku yake ya kuzaliwa. Kwa Euro 2,000 hiyo ina maana Nikky, alinyoa kichwa cha Balotelli kwa zaidi ya Sh 5 milioni.

“Lakini, hawa watu si kama wanalipa kwa kuwanyoa, wanajaribu kufanya utu tu na kunisaidia kwenye maisha yangu ya baadaye na familia,” alisema Nikky.

“Mitindo ya nywele ninayowanyoa haina thamani hiyo, lakini watu wamekuwa wakinitazama na kusema wamefurahishwa na kazi yangu. Wanasema sifeki maisha na kuwa mimi halisi, hivyo wanatoa kama sehemu tu ya kuwamasisha vijana kuwa na mtazamo chanya katika kila jambo.

Wanaamua kunisaidia kipesa na jambo hilo limekuwa likinigusa sana na kuwafurahia kwa utu wao.”

Advertisement