Kilichotokea mastaa walipozigomea klabu zao Ligi Kuu England

Muktasari:

Hata hivyo, Koscielny si mchezaji wa kwanza staa kwenye Ligi Kuu England kuingia kwenye mgomo wa kushinikiza auzwe na klabu yake.

LONDON,ENGLAND.ARSENAL imekuwa timu ya mwisho kwa siku za karibuni kujikuta kwenye kasheshe la kupambana na nguvu ya mchezaji.

Beki wa kati, Laurent Koscielny, nahodha wao, amepigwa faini na klabu hiyo baada ya kugomea kusafiri na timu kwenda Los Angeles kwenye kambi ya maandalizi ya msimu mpya.

Koscielny ameitisha mgomo huko Arsenal akitaka afunguliwe mlango wa kutokea, huku klabu za tatu za Ufaransa Bordeaux, Lyon na Rennes zikionyesha dhamira ya dhati ya kunasa huduma ya beki huyo wa kati mwenye umri wa miaka 33. Pia Barcelona inahusishwa na mpango wa kumnasa akazibe pengo la Samuel Umtiti endapo ataondoka katika dili la kubadilishana wachezaji na PSG ili Neymar atue Camp Nou. Koscielny amebakiza mkataba wa mwaka mmoja kwenye kikosi hicho na hivyo nataka Arsenal wamwachie aondoke bure.

Shida ni kwamba Arsenal wanahitaji kupata Pauni 10 milioni kwenye mauzo ya beki huyo, kwamba hawapo tayari kumwacha tu aondoke kitu ambacho kimewaingiza vitani na mchezaji wao Koscielny.

Ripoti zinadai kwamba beki huyo yupo tayari hata kuununua mkataba wake, ambao analipwa Pauni 90,000 kwa wiki ili tu aachane na Arsenal. Itakuwaje, Koscielny ataondoka kwa mgomo wake huo au Arsenal watakaza na kugoma kumwachia?

Hata hivyo, Koscielny si mchezaji wa kwanza staa kwenye Ligi Kuu England kuingia kwenye mgomo wa kushinikiza auzwe na klabu yake.

Riyad Mahrez

(Leicester City)

Staa wa Leicester City, Riyad Mahrez aliingia kwenye mgomo baada ya uhamisho wake wa kwenda Manchester City kugomewa.

Kilichotokea ni kwamba Mahrez aliingia kwenye mgomo kwa wiki mbili na kukosa mechi ya kwanza ya msimu mpya baada ya Leicester City kugoma kumuuza kwenda Man City. Hilo lilitokea kwenye dirisha la Januari mwaka jana.

Lakini, dirisha lilipofungwa Mahrez alibaki Leicester City hadi msimu ulipokwisha ndipo alipokamilisha ndoto zake za kwenda kujiunga huko Etihad kwa uhamisho wa Pauni 60 milioni. Mahrez anafurahisha maisha yake huko Etihad akifanikiwa kubeba pia ubingwa wa Ligi Kuu England.

Diego Costa

(Chelsea)

Straika Diego Costa aliamua kubaki zake Brazil wakati alipotibuana na kocha wa Chelsea, Antonio Conte. Alifanya hivyo wakati alitakiwa kurudi kwenye timu kuendelea na maandalizi ya msimu mpya. Kilichotokea ni kwamba Costa baada kupokea meseji kwenye simu yake kutoka kwa Conte akimwambia kwamba maisha yake ya kuichezea Chelsea yameshafika mwisho, straika huyo aliamua zake kubaki Brazil wakati alipokwenda likizo mwaka 2017.

Sawa, Chelsea ilimuadhibu Costa kwa kitendo hicho, lakini aliingia kwenye mgomo hadi alipoondoka kwenda Atletico Madrid kwa ada ya Pauni 57 milioni. Hadi leo Chelsea hawajapa mrithi wake kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati.

Carlos Tevez

(Man City)

Mshambuliaji wa Kiargentina, Carlos Tevez alizua utata huko Manchester City wakati alipomgomea kocha Roberto Mancini alipomtaka aingie kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich. Kitendo cha Tevez kumgomea kocha wake kuingia uwanjani kilimkera Mancini na hivyo wawili hao wakaingia kwenye mgogoro, uliomfanya Tevez kwenda kwao Argentina na hakurudi Man City akitaka aondoke moja kwa moja.

Tevez aligoma kwa muda mrefu kiasi cha kumfanya awe amepoteza Pauni 9.3 milioni kwa makato ya faini, mishahara na bonasi. Lakini, baadaye Tevez alirudi na kucheza timu hiyo kwa msimu mmoja na nusu kabla ya kuondoka moja kwa moja.

Dimitar Berbatov

(Tottenham)

Staa Dimitar Berbatov aliingia kwenye mgomo huko Tottenham Hotspur akiwashinikiza wamuuze kwenda Manchester United. Kama ilivyokuwa kwa Tevez, Berbatov naye aligoma kuingia kuichezea Spurs kwenye mechi ya ligi iliyopigwa nyumbani mwaka 2007.

Alichukia kwa kitendo cha kuwekwa kwenye benchi. Mgomo wa staa huyo ulimfanya akose mechi dhidi ya Sunderland na Chelsea, akiwalazimisha Spurs wamuuze kwenda Man United baada ya kuonyesha dhamira ya kutaka saini yake.

Hatimaye, Berba, alitimiza lengo lake baada ya kutua Old Trafford kwa ada ya Pauni 30.75 milioni jambo ambalo lilimkera sana mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy akisema Berbatov hakuwatendea heshima kabisa waliyostahili.

Kieron Dyer

(Newcastle)

Kocha Sir Bobby Robson aliingia kwenye mgogoro na staa Kieron Dyer baada ya mchezaji huyo kugoma kuchezeshwa kwenye kiungo ya kulia. Kilichotokea ni kwamba Sir Bobby Robson alimpanga Dyer kwenye kiungo ya kulia katika mechi ya kwanza ya msimu ambapo Newcastle United walikuwa wakiwakabili Middlesbrough mwaka 2004, lakini Mwingereza huyo aligoma.

Dyer alitaka achezeshwe kwenye kiungo ya kati na kupingana na matakwa ya kocha Robson. Jambo hilo lilimfanya Robson ampige benchi kiungo huyo, lakini akadai kwamba Dyer ni majeruhi. Taarifa zilipovuja, mashabiki wa Newcastle walichofanya wakawa wanamzoea Dyer hadi hapo alipoomba msamaha. Hata hivyo, mechi mbili baadaye, Robson akafutwa kazi. Hata hivyo Dyer anajutia kitendo chake.

Dimitri Payet

(West Ham)

Dimitri Payet alikuwa staa huko West Ham United, lakini mwaka 2017 aliishinikiza klabu hiyo imuuze. Kilichotokea ni kwamba West Ham United waligomea ofa ya Pauni 20 milioni kutoka Marseille waliyokuwa wakimtaka mchezaji huyo kipenzi chake, Jambo hilo lilimtibua Payet kwa sababu alitaka auzwe tu na hivyo aliripotiwa kuwaambia West Ham United kwamba hatapiga tena mpira akiwa kwenye kikosi chao.

Mwisho wa jambo hilo ni kwamba West Ham walikubali Pauni 25 milioni za Marseille na hivyo mchezaji huyo akatimkia zake huko na baada ya kuondoka tu, Payet alisema aliwapiga mkwara West Ham na wao waliogopa wakidhani kwamba angefanya alichosema kwamba asingecheza tena mpira.

Pierre van Hooijdonk

(Nottingham Forest)

Hii ilitokea mwaka 1998, kipindi hicho Nottingham Forest walikuwa wakikipiga kwenye Ligi Kuu England. Kilichotokea ni kwamba baada ya kurudi akitokea kwenye fainali za Kombe la Dunia 1998, staa Pierre van Hooijdonk aliwaambia Nottingham Forest anataka kuondoka, lakini timu hiyo iligoma kumuuza. Kutokana na hilo, Hooijdonk aliamua kurudi kwao Uholanzi na kwenda kufanya mazoezi na klabu yake ya zamani ya NAC Breda. Staa huyo alikuwa kwenye mgomo kwa wiki 12, kisha akarudi kwenye kikosi chao na kukishuhudia kikishuka daraja. Baada ya hapo, alipigwa bei kwenda Vitesse Arnhem huku Forest wakiishia tu kushuka daraja na tangu hapo Ligi Kuu England wamekuwa wakiisikia tu kwenye bomba.

George Best

(Man United)

Gwiji wa Manchester United, George Best aliondoka vibaya sana huko Old Trafford. Hii ilikuwa mwaka 1974, wakati Man United ikiwa nafasi ya tatu kutoka mkiani, Best hakuonekana mazoezini kwa sababu zake binafsi.

Alirudi kwenye timu, akatibuana na kocha Tommy Docherty, hivyo kocha akaamua kumpiga benchi staa huyo kitu ambacho kilimfanya aingie kwenye mgomo. Kocha Docherty hakuwa mtu wa mchezo mchezo, akamkata Best mishahara ya wiki mbili, kisha akamweka kwenye orodha ya wachezaji wanaouzwa, hapo ukawa mwisho wa gwiji huyo huko Old Trafford. Lakini, ndiyo hivyo, Best akaondoka zake kutoka kwenye kikosi hicho na Man United walikuwa kwenye wakati mgumu hakika.

Paul Scholes

(Man United)

Kiungo Paul Scholes amekuwa na hadhi kubwa huko kwenye kikosi cha Manchester United. Lakini, staa huyo wa Kiingereza kuna wakati alitibuana na kocha wake Sir Alex Ferguson. Kilichotokea ni kwamba baada ya kuwekwa benchi na Ferguson kwenye mechi ya kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Liverpool, mwaka 2001, kiungo Scholes alichukia na kugomea kucheza kwenye mechi dhidi ya Arsenal katika Kombe la Ligi.

Mechi hiyo ilimalizika kwa Man United kukumbana na kipigo cha mabao 4-0. Hata hivyo, jambo hilo lilimalizwa chini kwa chini na Ferguson akaanza kumtumia kwenye kila mechi Scholes na kufanikiwa kushinda mataji sita ya Ligi Kuu England baada ya hapo na taji moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Clint Dempsey

(Fulham)

Clint Dempsey akiwa staa mkubwa huko Fulham, mambo yalikwenda kombo mwaka 2012. Kilichotokea ni kwamba kiwango cha uwanjani cha staa huyo wa Kimarekani kilizivutia timu nyingi, zikaanza kumsaka kuanzia Liverpool, Aston Villa na Tottenham. Jambo hilo lilimfanya Dempsey kutaka kuondoka Fulham mwaka huo, lakini timu yake ikagoma ikitaka abaki. Dempsey akaamua kuingia kwenye mgomo na hakucheza mechi nne za mwanzo wa msimu mpya. Mpango huo ulikwenda vizuri kwa Dempsey ambapo mgomo wake uliishia kwenye kupigwa bei ambapo mshambuliaji huyo alikwenda kujiunga na Tottenham Hotspur Septemba kabla ya dirisha la usajili halijafungwa kwa ada ya Pauni 6 mil.