Kigogo Simba apigwa stop

Thursday August 13 2020

 

By Mwandishi Wetu

IKIWA ni siku chache baada ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa kujiuzulu nafasi hiyo na kuajiriwa Yanga, Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo imemsimamisha Mkurugenzi wa Wanachama wa Simba, Hashim Mbaga.

Mbaga alikuwa anafanya kazi ofisi moja ya Senzo na jana taarifa za kusimamishwa kwake zilianza kusambaa mitandaoni huku viongozi wa Simba wakithibitisha hilo.

Habari kutoka ndani ya Simba, zinasema kusimamishwa kwa mkurugenzi huyo ni kupisha uchunguzi wa baadhi ya mambo ambayo yamedaiwa kuwa tofauti na matarajio ya waajiri wake.

“Ni kweli amesimamisha kwani kuna mambo yanachunguzwa na tunataka kujiridhisha ndipo uamuzi wa mwisho ufanyike,” alisema Mjumbe huyo wa Bodi ya Wakurugenzi.

Kuhusu atakayeikaimu nafasi ya Senzo alisema; “Bado suala hilo linajadiliwa lakini mpaka sasa hakuna anayekaimu ingawa shughuli za klabu zinafanyika kama kawaida na watendaji waliopo. Utaratibu wa ajira ya CEO unafanyiwa kazi,” alisema.

Hata hivyo, Mwanaspoti ilipomtafuta Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ na Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Mwina Kaduguda simu zao hazikupokewa.

Advertisement

Advertisement