Kariakoo derby itanogeshwa na visasi

Friday July 10 2020

 

By Masoud Masasi, Mwanza

WINGA wa zamani wa Wekundu wa Msimbazi, Mnenge Suluja amesema mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga ambayo ni ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho itanogeshwa zaidi na visasi vya timu hiyo.
Winga huyo amesema visasi hivyo ni pale ambapo Yanga watataka kutinga fainali ili kupata nafasi ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya kukosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara uliobebwa na Simba.
Simba pamoja na kutwaa ubingwa wa ligi lakini wanautaka ubingwa wa kombe hilo lakini zaidi ni kulipa kisasi cha kufungwa mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na watani zao bao 1-0 huku mechi ya mzunguko wa kwanza wakitoka sare ya bao 2-2.
Mechi hiyo ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam itachezwa keshokutwa Jumapili katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam  ambapo kesho Jumamosi itapigwa mechi ya nusu fainali ya kwanza kati ya Sahare All Stars na Namungo uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Katika pambano lililopita la Ligi Kuu,Yanga iliwatandika Simba 1-0 ambapo pia wekundu hao wa msimbazi tayari wameshatwaa ubingwa wa mashindano hayo msimu huu.
Akizungumza na Mwanaspoti Online, Suluja amesema pambano hilo litakuwa tamu ndani ya uwanja kwani litakuwa la kisasi kwa timu hizo mbili kitu ambacho litanogesha burudani kwa watazamaji.
“Ni mechi ngumu sana, Yanga wameukosa ubingwa wa Ligi Kuu sasa wanataka kutwaa kombe hili na huku Simba wanataka kulipiza kisasi kwani walipoteza mchezo uliopita kitu ambacho kitaleta bonge la burudani,” amesema
“Itakuwa nusu fainali ya kibabe sana kikubwa niwaombe waamuzi watakaochezesha wajitahidi kuongeza umakini maana huu mchezo huwa unakuwa na mambo mengi hivyo wanatakiwa kuwa makini zaidi ya hapo tutategemea burudani kubwa,” amesema Suluja.
Amesema katika pambano hilo Yanga wanaweza kupata ushindi iwapo watafanya mashambulizi kupitia katikati kwani kuna shida kubwa kwa mabeki wa kati wa Simba.
“Erasto Nyoni na Pascal Wawa wanatakiwa kuwa makini kwani wanafanya makosa ya kizembe nina wasiwasi kama washambuliaji Yanga wakileta presha kubwa kwa kushambulia kwa nguvu basi mchezo unaweza ukawa mgumu kwa Simba, ” amesema Suluja.

Advertisement