Kapombe ahusika kifaa kipya Simba

BEKI mpya wa Simba, David Kameta ‘Duchu’ amefichua namna alivyopenda kuiga mbinu za Shomary Kapombe na kukiri zimempa ubora alionao kwa sasa mpaka akatua Msimbazi.

Duchu aliliambia Mwanaspoti anapenda zaidi aina ya uchezaji wa beki huyo, ikiwamo utulivu, mbinu, akili, kasi na kunyumbulika uwanjani.

Ingawa alikuwa na kigugumizi kuzungumzia usajili wake, alimzungumzia Kapombe ni beki ambaye kama si majeraha anaamini angefanya makubwa zaidi Ligi Kuu msimu uliomalizika.

“Kapombe ni beki ninayemkubali sana kwenye ligi kuu, nikiwa madaraja ya chini nilipenda kumwangalia anavyotumia akili katika kufanya kazi zake, mpaka kesho bado najifunza mengi kutoka kwake.”

“Ni beki mwenye uwezo wa kufunga na anatoa pasi za mwisho za mabao. Yaani ni adimu sana kumwona beki ananyumbulika hivyo, hii inaonyesha anajitunza na ni mtu wa mazoezi yanayompa pumzi,” alisema.

Hata meneja wake, Racho Clement alikiri Duchu atakwenda kwenye timu sahihi ambayo katika nafasi yake atakutana na mchezaji mzoefu Kapombe atakayemwelekeza kama mwalimu wa namna gani anaweza akafika mbali.

“Kwa umri wake Kapombe atakuwa mwalimu wake wa kumwelekeza ni namna gani ambavyo ataweza kufanya makubwa kwa klabu katika michezo yake,” alisema.