Kagere afunguka mambo mazito Simba SC

Muktasari:

Hivi karibuni ziliibuka taarifa zisizo kuwa mchezaji huyo raia wa Rwanda ameomba kuondoka Simba kutokana na kutopata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, ingawa mwenyewe amesisitiza sio za kweli.


Dar es Salaam. Mshambuliaji wa mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba, Meddie Kagere amesema hafikirii kuondoka licha ya kutocheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza, tofauti na taarifa zilizopo kuwa ameomba kuondoka kwenye klabu hiyo.

Katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu dhidi ya Ihefu SC mjini Mbeya, mchezaji huyo aliingia kipindi cha pili.

Kagere aliyekuwa kipenzi cha Kocha Patrick Aussems aliyetimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Sven Vandenbroeck, amekuwa akiingia uwanjani akitokea benchi katika mechi za karibuni ikiwamo zile za mwisho wa msimu uliopita.

Hivi karibuni ziliibuka taarifa zisizo kuwa mchezaji huyo raia wa Rwanda ameomba kuondoka Simba kutokana na kutopata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, ingawa mwenyewe amesisitiza sio za kweli.

“Niko vizuri, sina tatizo lolote na kutopata nafasi ya kucheza sasa inategemea, kwani mazoezi ndio yanampa mchezaji nafasi ya kupangwa kucheza, napambana na naamini siku moja nitarudisha namba yangu, ila niko vizuri, sina tatizo lolote,” alisema jana.

Akizungumzia madai kwamba ameomba kuondoka, mchezaji huyo alisema hajawahi kufikiria jambo hilo.

“Nina mkataba na Simba, naipenda Simba kuliko kitu chochote kwa sasa, nasisitiza tena niko sawa na ninaendelea kujifua kwa juhudi ili kusalia kwenye kiwango changu.”

Akimzungumzia Kagere, kocha wa zamani wa Simba, Salum Madadi alisema kuanzia benchi kwa mchezaji huyo katika mechi za hivi karibuni hakumaanishi kiwango chake kimeshuka, licha ya awali kuwa kwenye kikosi cha kwanza cha mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara.

“Picha kamili ya kiwango cha Kagere itaonekana kwenye mechi za ligi, lakini kwenye mechi za maandalizi ya msimu huwezi kumjaji, lakini kwa kawaida wachezaji wenye umri mkubwa kidogo huwa wanashuka viwango vyao kama hakuna msimamo kwenye mazoezi yao,” alisema Madadi.

Licha ya baadhi ya wadau kueleza kuwa kutowika kwa Kagere hivi sasa kwenye kikosi cha Simba ni kutokana na mfumo wa timu hiyo baada ya usajili wa dirisha kubwa uliomalizika hivi karibuni, Madadi alisema sio kweli.

“Mchezaji kuanzia benchi ni maoni ya kocha, lakini sio kama kiwango kimepungua, kocha kipindi cha mwanzo wa msimu huwa na mambo mengi katika kuimarisha kikosi.”

Aliongeza kuwa, “kwa Kagere bado yuko vizuri, ila kama anataka kubaki kwenye kiwango bora lazima utaratibu wake wa mazoezi uwe mzuri zaidi, akizembea kidogo basi atayumba na sio kwa Kagere tu, kwa mchezaji yeyote ambaye ana umri mkubwa kidogo.

“Tofauti na wenye umri mdogo ambao umri wao ni mkubwa kidogo, kama mazoezi hajakolea, programu haziko sawa na kuna kitu katika staili ya maisha hakiko sawa, hawezi kubaki kwenye kiwango chake.”