Kagera yatibua dili Yanga

Sunday August 02 2020
kagera pic

DILI limebuma. Wakati Yanga ikitajwa kuwa mbioni kumalizana na Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime pamoja na nyota watatu wa timu hiyo, mabosi wa klabu hiyo wametibua mambo baada ya kuamua kuwasainisha fasta ili kuwazuia wasitue Jangwani.

Kwa muda mrefu Yanga ilikuwa ikihitaji saini ya Maxime na Mwanaspoti linafahamu wazi hadi msimu wa 2019/2020 unamalizika, Kocha huyo tayari alikuwa na mkataba wa awali akisubiri mambo madogo yakamilishwe.

Kama haitoshi, Yanga walikuwa na mpango wa kuwabeba nyota watatu, ikiwa ni Yusuph Mhilu, beki wa kushoto David Luhende na Kipa Ramadhan Chalamanda.

Habari kutoka ndani ya Kagera zinadai kuwa tangu juzi Ijumaa, mabosi wa klabu hiyo ya Bukoba, walikuwa na kikao kizito na baadhi ya nyota wao na Maxime katika kuwaongeza mikataba.

Katibu Mkuu wa Kagera Sugar, Ally Said alithibitisha kumalizana na baadhi ya Mhilu, Luhende na Chalamanda kwa kila mmoja kusaini kandarasi ya miaka miwili sawa na Maxime.

Said alifafanua wachezaji hao pamoja na Kocha wao walikaa meza moja na kujadiliana kwa siku nzima kutokana na ofa walizokuwa nazo na kufikia hatua ya kumalizana nao wote.

Advertisement

“Nikutoe wasiwasi na hili lieleweke, ni kweli Kocha na wachezaji hao (Mhilu, Luhende na Chalamanda) walikuwa na ofa lakini jana (juzi) tulikuwa bize nao na tulifanikiwa kuwasainisha mikataba mipya na watakuwapo kikosini misimu miwili ijayo” alisema Katibu huyo.

Alieleza kuwa wachezaji ambao walishindwana kuongeza mikataba na kufikia hatua ya kuwaruhusu kuondoka ni Awesu Awesu aliyetimkia Azam na Zawadi Mauya aliyeenda Yanga.

Alisema msimu uliopita licha ya kutomaliza nafasi tatu za juu kama walivyokuwa wameazimia, lakini wamefanya vizuri na kwamba uongozi utarekebisha mapungufu yaliyoonekana ili msimu ujao wasikose nafasi hizo.

“Awesu na Mauya walikuwa na ofa kubwa na nzuri sana ambazo tulishindwa kuzifikia na tuliwaruhusu kwa baraka zote, hivyo uongozi tunaendelea kutengeneza kikosi kipya kwa kuzingatia ripoti ya Kocha” alisema Bosi huyo.

Advertisement