Kagera yaikaba Simba nje, ndani

Wednesday May 15 2019

 

By Thobias Sebastian

NI kama hadithi ya mbwa kwa chatu. Simba wanatisha msimu huu wakizifunga hadi timu kubwa barani Afrika katika Ligi ya Mabingwa, lakini mjanja wao yuko mkoani Kagera.

Simba wamepoteza mechi zote mbili za Ligi Kuu ya Bara msimu huu dhidi ya Kagera Sugar, na kuwa timu pekee iliyowafunga Wekundu wa Msimbazi nje, ndani na moja ya timu mbili tu zilizowafunga mabingwa hao watetezi katika Ligi Kuu msimu huu pamoja na Mbao FC ya Mwanza.

Kagera ndiyo timu pekee iliyowafunga Simba kwenye ligi kwenye uwanja wa nyumbani, ambao Ofisa Habari wao, Haji Manara, amekuwa akitamba kwamba hata mabingwa wa Hispania, Barcelona wakija na Lionel Messi wao, wanakufa.

Simba mbali ya kupoteza mechi zote mbili mikononi kwa Kagera Sugar msimu huu, msimu uliopita katika mchezo wa mzunguko wa pili Simba kwenye Uwanja wa Taifa walikubali kichapo cha bao 1-0, lililofungwa na Edward Christopher, mchezaji wa zamani wa Simba.

Kagera mbali ya kuwa na matokeo mazuri katika mechi tatu mfululizo walizokutana na Simba, lakini kila wanapokutana kuna mambo ambayo hutokea katika mchezo wao huo.

Makala haya yanakuleta baadhi ya mambo ambayo yamejitokeza katika mechi ya Simba dhidi ya Kagera Sugar.

Advertisement

KUNG’OA VITI

Mwaka 2013, goli la kusawazisha la penalti katika dakika ya mwisho la Kagera Sugar dhidi ya Simba lilizua kizaazaa kutoka kwa mashabiki waliodaiwa kuwa wa miamba hao wa soka nchini walioanza kung’oa viti na kurusha vitu mbalimbali uwanjani na kuwalazimisha polisi kutumia mabomu ya machozi kuwasambaratisha katika mechi iliyoisha kwa sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao kipindi cha kwanza lililofungwa na mshambuliaji Amissi Tambwe ambaye kwa sasa yupo katika timu ya Yanga na lilidumu hadi katika dakika za lalasalama kabla ya mchezo kumalizika.

Wakati Simba wakiamini mechi ingemalizika matokeo yakiwa 1-0, kiungo George Kavilla wa Kagera alipenyeza pasi ndefu kwa Daudi Jumanne aliyekuwa katikati ya mabeki wa Simba ndani ya boksi na beki wa kati Mganda Joseph Owino alimdondosha Jumanne aliyekuwa anataka kupiga shuti katika dakika ya tatu kati ya nne zilizoongezwa na mwamuzi wa akiba.

Kutokana na faulo hiyo, refa Mohamed Theofile kutoka Morogoro aliamuru kuwa ni ‘tuta’ lililofungwa na beki wa zamani wa Simba, Salum Kanoni.

Baada ya goli hilo kufungwa, washabiki wa Simba walianza kung’oa viti vya Uwanja wa Taifa kwenye Jukwaa la Simba lililopo Kaskazini mwa uwanja hali iliyowalazimu polisi kufyatua mabomu ya machozi na kuufanya uwanja huo kugeuka kuwa wa vita.

KWENDA FIFA

Msimu wa 2016-17, mechi ya mzunguko wa pili iliyochezwa Aprili 2, Kagera Sugar dhidi ya Simba ilipigwa katika Uwanja wa Kaitaba na wenyeji walishinda mabao 2-1.

Mara baada ya mchezo huo kumalizika Uongozi wa Simba chini ya Rais wake Evance Aveva walikata rufaa kupinga ushindi huo wa Kagera Sugar kuwa walimchezesha beki wa kati Mohammed Fakhi mwenye kadi tatu za njano na kuamua kwenda Shirikisho la soka la Dunia (FIFA) kudai pointi zao.

Uamuzi wa Kamati ya Sheria ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambao awali uliwapa Simba pointi tatu kuonekana kuwa na haki, ulipinga uamuzi huo na kurudisha pointi kwa Kagera Sugar ambao walionekana kuwa na haki kutokana na ushahidi uliotolewa.

Uongozi wa Simba mbali ya kuendelea kupinga ushindi huo wa Kagera kwa madai Fakhi hakuwa na haki ya kucheza mchezo huo, na hata kugomea zawadi ya mshindi wa pili waliyopewa katika mechi ya mwisho dhidi ya Mwadui walioshinda mabao 2-1, matokeo yalibaki vilevile kwa Yanga kuwa bingwa kwa kumzidi Simba mabao ya kufunga na kufungwa baada ya wote walimaliza na pointi sawa 68.

JPM AWAPA UKWELI

Mei 19, mwaka jana ni siku ambayo Simba wanaweza wasiisahau walipokabidhiwa kombe la ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kulikosa kwa miaka mitano likibebwa na mahasimu wao Yanga na Azam.

Simba siku hiyo waliingia na rekodi ya kutokupoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu Bara na walikuwa wanacheza dhidi ya Kagera Sugar huku mgeni rasmi akiwa Rais wa Jamhuru ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli.

Katika hali isiyotarajiwa Simba ilipoteza mchezo kwa kufungwa bao 1-0, huku penalti yao iliyopigwa na Emmanuel Okwi ambayo ingetosha kuwapa sare, ikiishia mikononi mwa kipa maarufu kwa kufuta penalti Juma Kaseja, kipa wao wa zamani, ambaye sasa yupo katika kikosi cha KMC.

Mara baada ya mchezo kumalizika kabla ya Simba kupewa zawadi zao kama kombe, medali, hundi ya pesa na nyingine, Rais Magufuli aliwambia ukweli kuwa kwa mpira ambao waliocheza hawawezi kufika popote kwani timu yao ni kubwa lakini haikuonyesha mpira kama lilivyo jina lao.

Magufuli pia aliwapongeza Kagera kwa kucheza vizuri na ‘kuwatoboa tobo’ mabingwa hao.

Advertisement