KPL yaanza kusaka sponsa mpya wa ligi

Muktasari:

Kulingana na Afisa Mauzo Mkuu wa KPL, Elly Kalekwa ambaye pia ndiye mmiliki wa klabu ya Sofapaka, kikao hicho kitakuwa cha kusaka mawazo ya wapi kumpata mdhamini mpya, kiasi gani cha pesa kitakachokuwa kinatolewa kwa kila klabu, kila mwezi na utaratibu wa kuanza msimu mpya.

BODI inayoendesha Ligi Kuu nchini KPL itafanya inapania kufanya kikao cha dharura kitakachowahusisha wenyekiti wa klabu zote ligini ajenda kubwa ikiwa ni kumsaka sponsa mpya kufuatia kujitoa kwa Sportpesa.

Afisa Mkuu Mtendaji wa KPL, Jack Oguda wiki iliyopita alitangaza kwamba huenda msimu mpya wa Ligi Kuu ulioratibiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu Agosti 31, utakosa kung’oa nanga baada ya hatua hiyo ya Sportpesa kujikata baada ya kunyimwa leseni ya kufanya biashara nchini na serikali.

Na huku kukiwa na hofu hiyo, KPL na wadau wake wameanza mchakato ya kumsaka mdhamini mpya wa kuwaokolea maisha.

Kulingana na Afisa Mauzo Mkuu wa KPL, Elly Kalekwa ambaye pia ndiye mmiliki wa klabu ya Sofapaka, kikao hicho kitakuwa cha kusaka mawazo ya wapi kumpata mdhamini mpya, kiasi gani cha pesa kitakachokuwa kinatolewa kwa kila klabu, kila mwezi na utaratibu wa kuanza msimu mpya.

Sportpesa waliokuwa wadhamini wakuu wa ligi hiyo walikuwa wakitoa Sh90 milioni kila mwaka na sasa baada yao kujitoa mambo ni magumu kinoma.

“Kupitia kikao hicho tutaamua namna msimu mpya utaanza, jinsi ulivyoratibiwa au itakuwaje. Naamini msimu utaanza jinsi tu ilivyoratibiwa kwa sababu hata kabla ya Sportpesa ligi ilikuwa inaendelea. Sasa hivi mipango yetu imevurugika ila naamini tutapata suluhu. Tayari tumeongeza juhudi ya kumsaka mdhamini mpya,” kasema Kalekwa.

Tayari mipango ya kuchezwa kwa Super Cup kama mechi ya ufunguzi ya msimu mpya Jumapili hii ipo palepale ambapo mabingwa wa Gotv Shield Bandari FC watakutana na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Gor Mahia uwajani uwanjani Machakos.