Jezi mpya zaipa nuksi Chelsea

Muktasari:

  • Chelsea inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England ikiwa na pointi 54

London,England. Nembo ya namba tatu iliyopo katika jezi mpya za Chelsea, zinaweza kutafsiriwa kama ni mkosi baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 3-2 na West Ham ikizitumia kwa mara ya kwanza jana.
Jezi hizo mpya ambazo zitatumiwa na Chelsea msimu ujao, zina nembo ya namba tatu ambayo ni ya kampuni ya Three UK inayojihusisha na utengenezaji wa simu huko Uingereza.
Kampuni hiyo ya Three UK ndio itakuwa mdhamini mpya mkuu katika jezi ya Chelsea baada ya mkataba baina ya klabu hiyo na kampuni ya matairi ya Yokohama kumalizika mwezi uliopita.
Timu hiyo ilianza kuzivaa jezi hizo kwa mara ya kwanza, juzi kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya West Ham lakini ikajikuta ikipokea kichapo cha mabao 3-2 ambacho kinahatarisha uwezekano wao wa kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
Katika mchezo wa jana, Chelsea licha ya kutoka nyuma na kusawazisha mabao mawili, ilijikuta ikifungwa bao la dakika za lala salama ambalo liliipa ushindi West Ham
West Ham ilipata mabao yake kupitia kwa Soucek, Michail Antonio na Andriy Yarmolenko wakati mabao mawili ya Chelsea kwenye mechi hiyo yakipachikwa na Willian.
Matokeo hayo yanaifanya Chelsea inayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England, kuwa mbele ya Manchester United waliopo nafasi ya tano kwa utofauti wa pointi mbili tu.
Utofauti huo wa pointi ni sawa na ule baina ya Chelsea na Wolves waliopo nafasi ya sita lakini pia wanawatangulia Arsenal walio nafasi ya saba kwa tofauti ya pointi nane.
Baada ya mchezo huo kocha wa Chelsea, Frank Lampard amesema wachezaji wake walimuangusha kwa asilimia kubwa.
"Sio jambo la kushangaza sana, kwa kuwa matokeo haya yamewahi kutokea kwenye michezo kadhaa iliyopita. Tulikuwa na nafasi ya kutumia mianya waliyoiacha na kuwafunga lakini hatukufanya hivyo.
Hii ni ishara ya kwamba kwa nini tupo hapa, na klabu kama
 Liverpool na Manchester City zinaonekana kuwa juu yetu, ni kwa sababu ya mwendelezo mzuri wa matokeo waliyonayo.
Kama haujapata takwimu nzuri kwenye mechi kubwa ni kweli kwamba lazima utaangusha pointi. Nafikiri tunahitaji kuwa na mwendelezo wa matokeo  mazuri ingawa tunaonekana kucheza vizuri katika baadhi ya  mechi. Wachezaji wanahitaji kuonyesha jitihada zaidi ili tushinde mechi," alisema Lampard.