Huyu Ntibazonkiza atawakera

KIRAKA mpya wa Yanga, Said Ntibazonkiza ameweka wazi kuwa Kocha Cedrick Kaze ndiye aliyemshawishi asaini Jangwani aje kumrahisishia kazi. Kaze anatua nchini kesho saa 4 usiku.

Mwanaspoti fasta likamuibukia mafichoni na kuzungumza naye ambapo, ametamba atatumia ujuzi wake wa kupiga faulo, chenga na kufunga magoli na kuzikera timu pinzani ili kuing’arisha Yanga.

Pia akasisitiza kuwa; “Nimekuja kufanya kazi na miguu yangu itaongea, vile nilivyo kwenye mitandao nitawaonyesha uwanjani.”

Saido alisema usajili wake Yanga ni maalum kwa kazi ya kurejesha heshima na furaha kwa mashabiki.

Winga huyo amesaini miaka miwili Yanga na jana akarejea kwao Burundi kwa majukumu ya timu ya Taifa na atatua nchini Novemba 15 kuungana rasmi na wenzake.

“Ilikuwa nisaini muda mrefu sana, lakini kuna mambo niliwaomba wasubiri na walinisikiliza. Tulifanya mazungumzo miezi mitatu iliyopita,” alisema winga huyo aliyeachana na VitalO ya Burundi kwa ishu za maslahi.

Said, 33, alisema alikuwa akiwasiliana na Kaze na alimwambia akifika Tanzania viongozi wa Yanga watamtafuta na ndio kilichotokea na kazi ikamlizika fasta tu.

“Niliposaini Kaze akanipigia kunipongeza na kuniambia anataka nifanye kazi maarufa ili kuipa timu mafanikio. Kaze anamheshimu sana na nilipokea maelekezo yake,” alisema Saido ambaye aliiua Stars wikiendi iliyopita.