Hivi ndivyo mastaa walivyokula bata

Monday July 15 2019

 

LONDON, ENGLAND.KIPINDI cha likizo kwa wanasoka wa Ulaya kimeshakwisha. Sasa hivi, mastaa wengi wamesharudi kwenye vikosi vyao kujifua kwa ajili ya mikikimikiki ya msimu ujao, wakibaki wachache tu ambao wanaendelea kula bata kwa sababu zao tofauti.

Kuna wenye ruhusa ya timu zao, lakini kuna ambao wameamua kugomea kujiunga na timu zao wakilazimishwa kuuzwa kama ilivyotokea kwa Antoine Griezmann na inavyoendelea kwa sasa kwa supastaa wa Kibrazili, Neymar.

Lakini kwenye kipindi cha likizo mastaa walikula bata kwelikweli. Kilichokuwa kikifanyika ni mashindano tu ya kukodi boti za kwenda kufanya starehe baada ya msimu mrefu wa purukushani za uwanjani.

Cheki gharama walizolipa mastaa hao kwa kukodi boti hizo kwa wiki ili kwenda kuponda maisha. Pauni Moja ni sawa na Sh2,872.07 za Kitanzania kwa mujibu wa mtandao wa Oanda. Starehe gharama asikwambie mtu. Hivi ndivyo mastaa walivyokula bata baharini.

JAN OBLAK

Angels and Demons, Pauni 23,000 kwa wiki

Advertisement

Kipa huyo wa Atletico Madrid, Oblak alihitaji kujipumzisha baada ya mambo magumu kwenye La Liga msimu uliopita. Kipa huyo aliamua kwenda zake huko Ibiza kwenda kuponda raha na mrembo wake, wakikodi boti iliyofahamika kwa jina la Angels and Demons.

Boti hiyo yenye urefu wa futi 73.03 iliyotengenezwa mwaka 2010 ina uwezo wa kuingia wageni sita kwenye vyumba vitatu tofauti, huku ikiwa na mambo mengi ya kisasa ikiwamo Wi-Fi. Kuna chumba cha VIP pia na gharama yake ya kukodi kwa wiki ni Pauni 23,000.

MANUEL NEUER NA MARIO GOTZE

Baloo 1 Pershing 74X, Pauni 35,000 kwa wiki

Wakati mastaa wa soka wa Ujerumani, Neuer na Gotze walipoamua kuwachukua wake zao warembo Ann Kathrin Brommel na Nina Weiss kwenda kula nao bata la likizo, walihakikisha wanafanya hivyo kwa kukodi boti moja ya kifahari matata kabisa.

Wakali hao waliamua kwenda kujipumzisha huko kwenye visiwa vya Balearic na kukodi boti iliyofahamika kwa jina la Baloo 1, ambayo gharama yake ya kuikodi kwa wiki ni Pauni 35,000. Mastaa hao waliamua kujipumzisha baada ya mchakamchaka wa msimu mzima kwenye Bundesliga.

RAHEEM STERLING

Golden Touch, Pauni 24,000 kwa wiki

Mwanasoka bora wa mwaka wa waandishi wa habari kwenye Ligi Kuu England, Raheem Sterling, aliamua kujipa mwenyewe raha baada ya kwenda zake Miami, Marekani mwezi uliopita. Sterling alitoka kwenye mtoko huo kabla ya klabu yake ya Manchester City kuanza kampeni ya maandalizi ya msimu mpya.

Katika bata lake, Sterling alikodi boti iliyofahamika kwa jina la Golden Touch ambayo mara nyingi imekuwa ikitia nanga huko Fort Lauderdale, Florida.

Boti hiyo iliyotengenezwa mwaka 1992 kabla ya kufanyiwa maboresho mwaka 2014 ni ya kisasa kwelikweli na gharama yake ya kuikodi kwa wiki ni Pauni 24,000.

KYLE WALKER

Cala Di Luna, Pauni 30,000 kwa wiki

Staa mwingine wa Manchester City, ambaye hakutaka kabisa kujinyima kwenye likizo yake. Beki wa kulia, Kyle Walker alikodi boti iliyofahamika kwa jina la Cala Di Luna na kwenda kula nayo bata akiwa na mrembo wake matata, Annie Kilner.

Walker alifanya mtoko huko ili kuboresha penzi lake baada ya Mei kuripotiwa kuachana na mrembo huyo baada ya kudaiwa kuchepuka, lakini mwezi uliofuatia, yaani Juni wawili hao walirudisha penzi kama ndio kwanza linaaza. Boti aliyokodi Walker malipo yake kwa wiki ni Pauni 30,000 na hakika si pesa ndogo kustarehe.

DALEY BLIND

Wajer 38, Pauni 20,000 kwa wiki

Staa wa Ajax, Mdachi Daley Blind alikuwa na msimu bora kabisa huko Ajax, akiisaidia timu hiyo kushinda mataji mawili ya ndani ya Uholanzi na kufika nusu fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Blind amekwenda kuonyesha kiwango bora baada ya kuonekana si kitu huko Manchester United.

Kiraka huyo aliamua kwenda zake kwenye fukwe za Amalfi akiwa na mpenzi wake, mrembo Candy-Rae Fleur. Wapendanao hao kwenye mtoko wao huko walikodisha boti ambayo iliwagharimu Pauni 20,000 kwa wiki na kwa siku walikuwa wakilipa Pauni 2,500 walipohitaji kufanya hivyo. Hivi ndivyo Blind alivyojiachia.

KEVIN-PRINCE BOATENG

Boom Shakalaka, Pauni 47,000 kwa wiki

Staa Kevin-Prince Boateng anapenda kula mambo mazuri bana. Katika likizo yake hakutaka kujinyima furaha baada ya kwenda zake huko Ibiza kula bata. Katika kuhakikisha mambo yake yatakuwa supa, staa huyo wa zamani wa Portsmouth alikodisha boti iliyoitwa jina la Boom Shakalaka.

Boti hiyo ina mambo mengi sana ya kisasa, huku ikiweza kuhimili mawimbi kwenye bahati jambo lililomgharimu staa huyo wa kimataifa wa Ghana Pauni 47,000 kwa wiki kutokana na kuikodi. Staa huyo alikuwa na marafiki zake wakila bata kabla ya purukushani za msimu mpya kuanza na kuwa bize na mambo ya uwanjani.

MAURICIO POCHETTINO

Shaka Princess V 58, Pauni 20,600 kwa wiki

Kocha wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino aliamua kusahau kipigo cha fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kutoka kwa Liverpool kwa kwenda kujipumzisha na mkewe mrembo Karina na watoto wao wa kiume Sebastiano na Maurizio huko Formentera.

Familia hiyo ilionekana ikiwa na furaha kubwa wakati walipokuwa ndani ya boti ya kifahari iliyofahamika kwa jina la Shaka Princess V 58.

Boti hiyo kwa siku kuikodi ni Pauni 3,000, lakini kwa wiki, Pochettino alilipa Pauni 20,600 na kufurahia maisha huku ikiwa na uwezo wa kuchukua abiria hadi 11, hivyo alipata starehe kwa kujinafasi kabisa kwenye likizo yake.

HARRY MAGUIRE

AB Yacht 58 Kanamo, Pauni 22,750 kwa wiki

Jina lake linatajwa usiku na mchana huko Manchester United, lakini beki wa kati Harry Maguire wala hakutaka mambo hayo ya usajili yatibue mipango yake ya kwenda kula raha katika kipindi chake cha likizo. Beki huyo wa Leicester City aliamua kukodi boti ya kifahari ya Kanamo, ambayo imedaiwa kuwa na mambo mengi ya kiburudani unapoikodi.

Hata hivyo, Maguire alijipanga vyema kwenye kufurahia likizo yake kwani boti aliyokodi ilimgharimu Pauni 2,600 kwa wiki, huku wiki nzima alikuwa akilipa Pauni 22,750 kufanya starehe na kufurahia maisha yake kabla hajafahamu kuhusu hatima yake ya msimu ujao huko England.

DELE ALLI

Delhia, Pauni 40,000 kwa wiki

Unapokuwa mchezaji unayelipwa Pauni 100,000 kwa wiki, jambo la kutumia pesa unapokuwa na mrembo matata haliwezi kuwa tatizo. Staa wa Tottenham Hotspur, Dele Alli alimchukua mpenzi wake Rub Mae na kukodi boti iliyoitwa Delhia kwenda kuponda raha huko St Tropez.

Boti hiyo ina mambo yote yenye kufurahisha na kukufanya usihisi upweke na ndiyo maana ilimgharimu staa huyo wa kimataifa wa England, Pauni 40,000 kwa wiki. Dele alihitaji kuwa na muda mzuri wa kuboresha penzi lake baada ya siku za karibuni kudaiwa kulegalega huku mtoko huo uliendana na siku ya kuzaliwa ya Ruby.

CRISTIANO RONALDO

Benetti Africa I, Pauni 180,000 kwa wiki

Asikwambie mtu, mwenye pesa siyo mwenzako. Cristiano Ronaldo alitaka kuonyesha kwamba yeye ni mtu mwenye mkataba wa maana baada ya kwenda kula bata huko kwenye visiwa vya Ugiriki na kisha French Riviera akiwa kwenye boti iliyofahamika kwa jina la Africa I, ambayo imedaiwa kuwa na thamani ya Pauni 15 milioni.

Boti hiyo ambayo ndani yake kuna mambo mengi ya kufurahia, ikiwamo Jacuzzi. Ndani ya boti hiyo kuna ukumbi wa sinema. Ronaldo alienda kula bata akiwa na mchumba wake, mrembo Georgina Rodriguez. Boti hiyo ambayo Ronaldo alikodi ilimgharimu Pauni 180,000 kwa wiki.

Advertisement