Haya ndio maajabu ya fainali za Kombe la Afrika

Tuesday July 23 2019

 

By Charles Abel

Dar es Salaam. Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka huu zimefikia tamati nchini Misri, juzi Ijumaa ambapo Algeria imemaliza ikiwa bingwa, baada ya kuichapa Senegal bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali.

Ushindi huo dhidi ya Senegal unaifanya Algeria iwe imetwaa taji hilo mara mbili, ubingwa wa kwanza ikichukua mnamo mwaka 1990 wakati fainali hizo zilipofanyika nchini mwao.

Mbali na Algeria kutwaa ubingwa, kumekuwa na timu, wachezaji na waamuzi waliofanya vyema kwenye vipengele mbalimbali lakini wapo ambao wamechemsha katika mashindano hayo ya mwaka huu kutokana na sababu moja au nyingine.

Tathmini ya jumla ya mashindano ya Afcon za mwaka huu kwa kuainisha vinara na waliochemsha kwenye vipengele mbalimbali na kuainisha takwimu na badhi ya rekodi zilizowekwa kwenye mashindano hayo mwaka huu.

Mchezaji Bora-Ismael Bennacer (Algeria)

Kiungo wa Algeria mwenye umri wa miaka 21, Ismaer Bennacer ameibuka mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa mashindano ya Afcon mwaka huu kutokana na kiwango bora alichoonyesha katika fainali hizo.

Advertisement

Dalili za Bennacer kutwaa tuzo hiyo zilianza kujionyesha mapema baada ya kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa mechi mara mbili mfululizo katika michezo ambayo Algeria ilicheza dhidi ya Kenya na Senegal kwenye hatua ya makundi.

Mfungaji Bora-Odion Ighalo (Nigeria)

Mabao matano ambayo mshambuliaji wa Nigeria, Odion Ighalo ameyafunga katika fainali hizo yamemfanya aibuke mfungaji bora wa jumla wa mashindano na kutwaa tuzo ya kiatu cha dhahabu.

Ighalo amefunga mabao hayo katika mechi dhidi ya Burundi, Cameroon, Algeria na Tunisia.

Kipa Bora- Rais M’bolhi (Algeria)

Kitendo cha kucheza mechi zote saba (7) za mashindano bila kufanyiwa mabadiliko na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu, kimembeba mlinda mlango wa Algeria, Rais M’bolhi ambaye ametajwa kuwa mshindi wa tuzo ya kipa bora wa mashindano.

Lakini pia mbali na kiwango bora na kucheza kwa dakika nyingi ambazo ni 660, M’bolhi ndiye kipa aliyedaka idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu bao kuliko mwingine yeyote ambapo nyavu zake hazijatikiswa kwenye mechi tano (5) za mashindano hayo.

Tuzo ya uungwana- Senegal

Timu iliyoondoka na tuzo ya uungwana kwenye mashindano (Fair Play Award) ni Senegal ambao katika mechi saba walizocheza kwenye mashindano hayo, wamepata kadi 10 tu ambazo zote ni za njano ikiwa ni wastani wa kadi 1.43 kwa mechi.

Utovu wa nidhamu- Benin

Timu iliyoongoza kwa utovu wa nidhamu ni Benin ambayo katika mashindano hayo ndio imepata idadi kubwa ya kadi kuliko timu nyingine yoyote ambazo ni kadi 17.

Katika idadi hiyo ya jumla ya kadi 17, kadi za manjano ni 15 na kadi nyekundu ni mbili ambazo zilionyeshwa kwa wachezaji Khaled Adenon na Olivier Verdon.

Fainali ya tano ya Wazawa

Kwa kitendo cha Senegal na Algeria zilizoingia fainali kunolewa na makocha Aliou Cisse na Djamel Belmadi ambao ni wazawa, fainali baina yao inakuwa ya tano kwenye fainali za Afcon kukukutanisha timu zinazonolewa na makocha wazawa tu.

Nne zilizopita ambazo zilikutanisha makocha wazawa ni Ethiopia dhidi ya Misri mwaka 1962, Ghana na Tunisia mwaka 1965, Ghana dhidi ya Uganda mwaka 1978 na nyingine ni ile ya mwaka 1998 kati ya Misri na Afrika Kusini.

Refa aliyetamba- Bamlak Tessema

Mwamuzi Bamlak Tessema Weyesa kutoka Ethiopia, ndiye refa wa kati aliyechezesha idadi kubwa ya mechi kuliko mwingine yeyote katika kundi la marefa 28 wa kati walioteuliwa kuchezesha mashindano hayo.

Tessema amechezesha mechi jumla ya mechi tano ambazo ni baina ya Senegal na Tunisia, Tunisia na Angola, Ghana na Cameroon, Algeria na Ivory Coast pamoja na ile iliyozikutanisha Senegal na Tunisia katika nusu fainali.

Mwamuzi aliyechemsha-Beida Dahane

Mwamuzi Beida Dahane kutoka Mauritania ndiye mwamuzi pekee wa kati ambaye hakuchezesha mechi hata moja za mashindano hayo tofauti na wenzake 27 ambao walipata fursa ya kushika kipyenga kwenye mechi mbalimbali za Afcon mwaka huu.

Idadi ya mabao

Jumla ya mabao 102 yamefungwa katika mechi 52 za mashindano hayo ikiwa ni wastani wa bao1.96 kwa kila mechi huku Algeria ikiwa kinara wa kufumania nyavu ikifunga jumla ya mabao 13.

Burundi ndio timu ambayo haijachangia chochote kwenye idadi hiyo ya mabao yaliyofungwa katika fainali hizo kwani haikuweza kupachika bao hata moja kwenye mechi zake tatu ilizocheza kwenye Afcon mwaka huu dhidi ya timu za Nigeria, Madagascar na Guinea.

Timu ya maajabu-Madagascar

Madagascar ilishiriki Fainali za AFCON 2019 ikiwa ni mara yake ya kwanza kama ilivyokuwa kwa Burundi, na Mauritania lakini wakati wenzake wakichemsha na kutolewa kwenye hatua ya mwanzo ya makundi, yenyewe ilifika hatua za mbali zaidi kwa kuondolewa kwenye Robo Fainali na Tunisia.

Ilimaliza hatua ya makundi pasipo kupoteza mechi hata moja ikipata ushindi katika michezo dhidi ya Nigeria na Burundi huku ikitoka sare na Guinea na kwenye hatua ya 16 bora ikaiduwaza DR Congo.

Senegal na mkosi wa penalti

Hapana shaka kwamba Senegal ndio timu iliyokuwa na nuksi na mapigo ya penati ambapo katika penalti nne ilizopata ndani ya muda wa kawaida wa mchezo ilipoteza penalti tatu.

Sadio Mane alipoteza penalti mbili moja dhidi ya Kenya na nyingine mbele ya Uganda na mwingine aliyekosa ni Salif Sane aliyekosa dhidi ya Tunisia.

 

Advertisement