Hatima ya Malinzi na wenzake Julai 23


Muktasari:

Wakili Richard Royongeza akishirikiana na jopo la mawakili wengine wa utetezi walidai hawana pingamizi kuhusiana na mabadiliko hayo.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Julai 23, 2019 imepanga kutoa uamuzi kwa aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Jamal Malinzi na wenzake kama wana kesi ya kujibu au lah.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya upande wa mashitaka kufunga ushahidi kwa mashahidi 15 kutoa ushahidi katika kesi hiyo.
Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai leo Ijumaa alidai mbele ya Hakimu Mkazi Maira Kasonde kuwa kesi hiyo ilipangwa kwaajili ya kusikilizwa lakini upande wa mashtaka wanategemea kufunga ushahidi.
"Kesi imepangwa kwaajili ya kuendelea na usikilizwaji, tunategemea kufunga ushahidi lakini tungeomba kufanya mabadiliko  ya baadhi ya maneno yaliyoko kwenye hati ya mashtaka chini ya kifungu 234," alidai Wakili Swai
Wakili Swai alidai baadhi ya maneno  yaliyoko katika shtaka la tatu na la nne ambapo awali yalikuwa yakisomeka muktasari wa kikao na badala yake yasomeke makubaliano ya kikao.
Aliongeza kuwa mabadiliko mengine ni shtaka la 18 ambapo badala ya kusomeka Oktoba 3, 2016 isomeke Septemba 26, 2016 na shitaka la 19 isomeke Septemba 26, 2016 badala ya Agost 24, 2016.
Wakili Richard Royongeza akishirikiana na jopo la mawakili wengine wa utetezi walidai hawana pingamizi kuhusiana na mabadiliko hayo.
Hakimu Kasonde alidai kwa kuwa ni swala ambalo liko kisheria ili kuweza kuendana na ushahidi uliotolewa na hakuna pingamizi na washtakiwa wanayo haki ya kutaka shahidi aliyetoa ushahidi kuitwa kuulizwa lolote au kutoa upya ushahidi chini ya kifungu cha 32(2)b.
Baada ya maelezo hayo Hakimu Kasonde aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 23 mwaka huu kwaajili ya washtakiwa kujua kama wana kesi ya kujibu au hawana.
Katika kesi hiyo mashahidi 15 wa upande wa mashitaka walitoa ushahidi katika kesi hiyo akiwemo Katibu Mkuu wa TFF,  Wilfred Kidao.
Mbali na Malinzi wengine ni Meneja wa  Ofisi ya TFF, Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya ambao kwa pamoja  wanakabiliwa na mashtaka 30 katika kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa USD 173,335.
Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wapo rumande wakikabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha kuwa miongoni mwa mashtaka ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana huku wenzao Zayumba na Frola wapo nje kwa dhamana.