Harmonize huyoo anakimbiza nje ya Wasafi kama utani

Sunday April 5 2020

Mwanaspoti, Tanzania, Harmonize anakimbiza nje, Wasafi Mbosso, Queen Darleen, Rayvanny, Lavalava, Diamond Platnumz

 

By CHARITY JAMES

HAKUNA aliyeamini Harmonize angeondoka WCB. Ndio, haikuwa rahisi ila sasa wengi wameshazoea kuona msanii Rajab Abdul ‘Harmonize’ au ukipenda  ‘Konde Boy’ kutoka Wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara akiondoka kwenye lebo hiyo.
Harmonize aliyeanza kutoka mwaka 2015 na ngoma yake ya ‘Aiyola’ alisaini mkataba na lebo kubwa ya muziki nchini Wasafi Classic Baby (WBC).
Lebo hiyo inayomiliki wasanii kama Mbwana Kilungi ‘Mbosso’ Mwajuma Abdul ‘Queen Darleen, Raymond Shaban ‘Rayvanny na Abdul Iddi ‘Lavalava inaongozwa na kamanda wao Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’.
Hata hivyo, baada ya tetesi kuvuma anataka kuachana na lebo hiyo, Harmonize ambaye alishaanza kupaa kisanii hasa kimataifa akaibuka na kukiri na kubwa akidai anataka kufanya mengi makubwa na kujitegemea.Katika kuthibitisha ukweli wa hilo, uongozi wa WCB ulithibitisha kupitia mmoja wa mameneja wa Diamond, Salam SK alisema Harmonize aliuandikia barua uongozi wa lebo hiyo akiomba kuondoka.
Salam anasema Harmonize alikuwa tayari kafuata sheria zote ili kuvunja mkataba wake na kuanza kufanya kazi mwenyewe chini ya lebo yake ya Konde Gang ambayo taratibu inaanza kukua.
Mambo yaliyokuja kuwathibitshia watu msanii huyo ameondoka kwenye lebo hiyo ni kuanzisha lebo yake ya Konde Gang kwa maana kanuni haziwezi kumruhusu mtu ambaye yuko chini ya lebo fulani kuingia katika lebo nyingine au kuanzisha pia.
Jambo lingine ni kutoonekana kwenye show za Wasafi Festival pamoja na mikutano yao ya waandishi wa habari au kwenye sherehe mbalimbali zinazojumusha wasanii wa lebo hiyo.
Msanii huyo ameanza kung’ara au kuota mbawa tangu kuondoka katika lebo hiyo na kwa kipindi cha mwezi mmoja tu tangu kuanza kwa tetesi za kujiondoka, msanii huyo ameweza kufanya mambo makubwa manne ambayo hakuna masanii aliyefanya baada ya kuachana na lebo hiyo.
Mwanaspoti linakuletea mambo hayo aliyoyafanya akiwa nje ya WCB ambayo yaliendeleza ubora wake katika tasnia ya muziki huo.

KUFUNGA NDOA
Kwa kipindi chote alichokuwa chini ya WBC, Harmonize alikuwa hajaoa lakini baada tetesi zikiwa bado za moto juu ya kuondoka kwake zilianza kuvuja picha mbalimbali akiwa kwenye mavazi ya harusi na mpenzi wake Sarah.
Licha ya kwamba harusi hiyo ilikuwa ya siri na hakuna msanii kutoka WCB aliyehudhuria, lakini Harmonize aliposti kwenye Instagram yake kwa hatua hiyo aliyofikia na baadhi ya wasanii na watu maarufu walimpongeza.
Mke wake Sarah alikuwa wa kwanza kuposti kwenye ukurasa wake wa Instagram kabla ya Konde Boy kujibu mapigo kwa kuposti pia kwenye ukurasa wake wa mtandao huo. Kwa hatua hiyo Harmonize amefanya jambo kubwa lenye heshima kwa jamii.

KONDE BOY MGAHAWA
Septemba 24 kupitia ukurasa wake wa Instagram, Harmonize alitangaza ujio wa Konde Boy Mgahawa. Alisema hivi karibuni litakuwa likipita gari maalumu lililopigwa logo ya Konde Boy ambalo litatoa vyakula bure mitaani.
Hiyo ni dalili tosha kwa msanii huyo yupo njiani kufungua mgahawa ambao kazi kubwa itakuwa ni kuuza vyakula baada ya ile awamu ya bure kumalizika, hiyo ni moja ya mafanikio ambayo ameyapata msanii huyo tangu kutoka WCB.
Kuna kila dalili msanii huyo alijipanga mapema kufanya makubwa hayo na inawezekana alikuwa akipanga hayo kabla hata ya kuachana na WCB.

TUZO ZA MTV
Harmonize aliingia anga za kimataifa baada ya kuwa msanii pekee kutoa Afrika Mashariki kuingia katika tuzo kubwa za MTV Europe Music Awards kwa mwaka 2019.
Katika tuzo hizo za MTV Europe Music Awards zilizofanyika Novemba 3, 2019, jijini London Uingereza, Harmonize alishindanishwa na wanamuziki kutoka Afrika Magharibi.
Licha ya kutopata tuzo hizo, Harmonize alifurahishwa na hatua hiyo na kuwaomba mashabiki kuendelea kumpa sapoti.

JUKWAA MOJA NA WIZKID, YEMI ALADE
Mwishoni mwa mwaka jana, Harmonize alisafiri mapaka Sydney Australia kwenye tamasha la A.P.E ambalo lilijumuisha wasanii wakubwa Afrika Yemi Alade na Wizkid.
Harmonize amefanya kolabo na Yemi Alade kwenye wimbo wa Show Me What You Got pamoja na ule wa Krizzbeatz alioshirikisha wasanii hao wote.
Ukiachana na Diamond Platnumz wasaii wengine waliowakilisha Afrika kimataifa ni pamoja na Wizkid hivyo kwa mara ya kwanza alikuwa naye kwenye jukwaa moja chini ya lebo yake ya Konde Gang.

KUZINDUA ALBAMU
Katika tukio hawezi kulisahau ni hili la uzinduzi wa albamu ya ‘Afro East’ ambalo limeshuhudiwa likiwa la kipekee kwa kuhudhuria na baadhi ya viongozi na mastaa.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria ni rais mstaafu Jakaya Kikwete, Waziri wa Habari, Harrison Mwakyembe na Naibu Spika wa Bunge Tulia Ackson.
Hii siku ya kipekee kwa msanii huyo ambaye maisha yake tangu kuachana na WCB yameonekana kutoyumba, huku akiendelea kuleta upinzani mkubwa upande wapili.

HITIMISHO
Harmonize amekuwa msanii wa pili kuacha na WCB baada ya msanii Richard Mavoko ‘Rich Mavoko’ kufanya hivyo miaka miwili iliyopita ambapo kwa sasa anajitahidi kusimamaisha lebo yake ya Billionaire Kid ambayo bado hajaanza kusajili wasanii kama ilivyo kwengine.
Hivyo hivyo ilivyo kwa msanii Harmonize hajaanza kusajili wasanii kwenye lebo yake ya Kond Gang na pengine kutokana na ukubwa wa msanii huyo anasubiri muda sahihi wa kuanza kufanya hivyo ili kupata familia yake baada ya kuhama nyumbani kwao.

Advertisement