Harmonize, Jux, Dimpoz wamewafunika Diamond na Ali Kiba

Tuesday December 3 2019

Harmonize- Jux- Dimpoz -wamewafunika -Diamond - Ali Kiba-ubalozi-kimapenzi-mabalozi-Afrika- Mashariki-burudani-Mwanasport-MwanaspotiSoka-MwanaspotiGazeti-

 

By Luqman Maloto na Dk Levy

KIMUZIKI wameona hawawawezi lakini kwani maisha yanaishia kwenye muziki? Harmonize, Jux na Ommy Dimpoz wamewafunika Diamond Platnumz na Ali Kiba kwa ubalozi wa kimapenzi. Diamond na Ali Kiba wenyewe ni mabalozi ndani ya Afrika Mashariki, Harmonize, Jux na Ommy wanawakilisha mbali, Italia, Thailand, Hispania. Ni mjadala kijiweni, Dk Levy na Luqman Maloto.

DK LEVY: Nilishakuonya sana tabia ya kukurupuka hata huelewi. Yaani hata saa nane usiku wewe unakurupuka tu. Hivi tabia ya kukurupuka utaacha lini?

LUQMAN: Tuliza mizuka wewe. Kwani muda huu si ndio Ali Kiba amemaliza kukiwasha Ali Hassan Mwinyi Stadium? Unajua nini? Ali mjanja sana, Unforgettable Tour kaianzia kwenye uwanja wa wajina wake. Ali Mwinyi, Ali Kiba.

DK LEVY: Siku hizi kumekuwa na shoo chache. Wasanii wachache. Matajiri wa muziki wachache. Yaani walewale wanatrend miaka yote tangu 2010. Ajabu ni kwamba mabaunsa ni wengi kuliko wasanii. Mameneja pia ni wengi kuliko idadi ya nyimbo za wasanii husika. Pia kufanana kumekuwa kwingi. Wasanii wa Kings Music usipokuwa makini unaweza kudhani nyimbo zote kaimba Kiba. Mpaka uvaaji wanaigana. Hata kutoka na mademu wa nje ya nchi wanaigana.

LUQMAN: Harmonize yeye ni wa kipekee, demu wake ni Muitaliano. Kaka zake wanakomaa na mademu wa Kenya na Uganda, yeye kaenda Italy. Halafu yule Jux komesha, ndio nini kum-replace Vanessa Mdee kwa demu wa Thailand? Madogo wanazurura sana kutafuta mademu kuliko kuzurura kutafuta pesa na michongo. Ommy Dimpoz amezaa na demu ya Hispania, Ben Pol kalowa kwa Anerlisa wa Kenya.

DK LEVY: Ila vijana wa Bongo kwa ngono za mbali hawajambo. Hivi yule Elizabeth Gupta aliyeolewa na mshindi wa BBA yule andunje wa Kinaijeria Kelvin, bado ndoa yao ingali hai? Huwa mnasahau sana kuwa Dola Sol a.k.a Balozi kaoa Mzungu wa Kimarekani. Pia Rama Dee kaoa na anaishi Australia huko na Mzungu wake. Pia Mr Paul naye yupo huko huko na Mzungu wake. Pia usisahau kuwa Zavara wa Kwanza Unit naye anaishi na Mzungu Canada. Yule sista duu Teddy Kalonga a.k.a ‘TK’ wa EATV naye yupo Marekani na Mzungu wake kitambo sana. Hata Millen Magesse (Happyness) kazaa na Mzungu sijui wa wapi.

Advertisement

Kifupi unapoona dem kama Sinta alikomaa na Juma Nature kipindi kile, Majizo na Diamond kuzaa na Mobetto, Elizabeth Michael Lulu kukomalia mbavu za Majizo, Aunty Ezekiel kuendelea kushea joto la Dar na Mose Iyobo, huo ndio uzalendo mkubwa sana sana sana kwa taifa. Wanastahili pongezi. Kina Lucy Komba, Saida Kessy, Miriam Odemba walishindwa kabisa kufanya huo ubwege.

LUQMAN: Ukitaka tuongee hivyo basi mamia kama si maelfu wameoana au kuunda familia na wapenzi wa mataifa mengine. Tunazungumzia wanamuziki wetu, ‘imajini’ Jux hajawahi kufanya shoo Thailand lakini ameng’oa demu wa Kithailand. Labda tuwashindanishe, nani katisha? Jux na Mthailand? Harmonize na Muitaliani. Ommy na Mspaniola. Diamond naye mechi zake zimezoeleka, ana watoto wawili na Mganda, mmoja na Mkenya, mmoja na Mtanzania. Bora Ben Pol yeye kang’oa mrembo tajiri Kenya, Zari anasubiri, hata akiunganisha mali za marehemu Ivan.

DK LEVY: Mpaka sasa ni Samatta na Diamond tu waliokanyaga mataifa mengi kwa ajili ya kazi zao. Hawa wengine wote waliishia Kericho hapo kama siyo Nakuru na Sirari. Unajua Mungu kuna wakati ukifika hutoa kipaji halisi kwa mtu. Ben Pol hana kipaji cha muziki na kifupi siyo mwanamuziki. Ila muziki umefanywa kama njia yake ya kuelekea kwenye kipaji chake maridhawa cha umarioo a.k.a uben ten wenye userengeti boy ndani yake.

Kulelewa ndo kipawa alichopewa na Mungu ndugu Benard Pol. Huku kuimbaimba ni kiherehere chake na jukwaa la kutazamwa na kunyakuliwa na wadada mafundi wa kulea masela.

Yeye Jux muziki ni kama basi la mwendokasi kwake, lakini kipawa chake kikuu alichojaaliwa toka tumboni kwa mama yake ni maisha ya ‘ulover boy’. Kulamba lips, kujipodoa mpaka madem wanamuogopa.

Vanessa Mdee nilimsikia anahojiwa sehemu akasema siku bishoo yule ‘anamuaprochi’ hakuamini. Na zaidi akawa amepewa adhabu kubwa sana ya kuanza kuhangaikia vipodozi na make up kama zote. Ili tu angalau afanane na dem anayetakiwa kutoka na bishoo kama Jux. Yule dogo ni bishoo mpaka anaufanyia ubishoo hata ule ubishoo wake mwenyewe.

LUQMAN: Mambo mengine nakukubalia lakini ukisema Ben Pol hana kipaji cha muziki nakukatalia, a big no. Yule janki ni fundi sana, sema siku hizi mapenzi yamemzidi nguvu. Jux ni mwanamuziki mkali bishoo, sikupingi. Kuna kitu najifunza, yule Steve Nyerere angekuwa anaweza kuzungumza lugha za kigeni, angedaka mademu wa kimataifa kuliko hao mabishoo wako. Steve ana ulimi laini ambao humwezesha kupenya pasipopenyeka.

DK LEVY: Ulimi wa Steve Nyerere unapenya kwa mapedeshee ambao hawapendi longolongo nyingi. Wakikutana naye tu akianza perere zake wanazama mfukoni wanampa mkwanja atulie. Sasa kama kuna madem mapedeshee sawa atawapata. Steve ni wale binadamu masalia wa kizazi cha Herode kutoka Uyunani kwenye milima Mizaituni, ambao walivunja mkataba na aibu. Wakatoa talaka kwa soni. Kisha wakanuniana na neno staha na hofu.

Yaani ni wale watu tunaosema hawana mshipa wa haya. Popote anaingia na yeyote anamuingia. Steve ni kama bakteria wa mafua. Wanaingia popote. Sema Steve anachojivunia ni jina lake kuanza kujulikana kabla ya Piere Liquid. Lakini ndo wale wale tu.

LUQMAN: Maajabu ya ulimwengu ni kuwa Steve Nyerere alivyo, yule Pierre Liquid akisimama na Steve Nyerere ni kama wewe ukisimama na Hasheem Thabeet. Kwa kifupi Steve Nyerere ni Hasheem Thabeet wa Pierre Liquid.

DK LEVY: Ila Wabongo tunaigana sana. Simba nao wamemtimua Uchebe aiseee. Kocha aliyewapa ndoo ya Ligi Kuu na kuwafikisha robo fainali Klabu Bingwa Afrika. Na timu kaacha ikiwa inaongoza kwenye msimamo wa ligi. Sasa naomba kuuliza ni timu ipi imebadilisha mfumo wa uendeshaji kati ya Simba na Yanga? Maana Yanga wamemtimua Papaa Zahera kwa matokeo mabaya. Simba wanamtimua Uchebe akiwa na matokeo mazuri.

Wabongo hatujui tunataka nini na hatutaki lipi. Ukishaona timu zinaajiri wapiga porojo wanaowaita ‘wahamasishaji’ ujue hapo hamna timu ila kuna genge la mchanganyiko wa binadamu wanaotaka kupiga hela tu duniani. Hawataki kuacha historia kama kina Mzee Bamchawi au Jabiri Katundu (RIP wote hao).

LUQMAN: Acha zako, kwa wastani mpaka sasa, msimu huu Yanga imefanya vizuri kuliko Simba. Yanga walifuzu raundi ya pili Klabu Bingwa Afrika wakati Simba iliondolewa raundi ya kwanza. Zingatia Simba ilijiandaa na mashindano, Yanga haikuwa na maandalizi yoyote, ilipata nafasi ya kushitukiza.

Angalia usajili wa Simba, tazama Yanga. Ligi Kuu Bara, Yanga imefungwa moja na kutoa sare mchezo mmoja. Simba pia imefungwa moja na kutoa sare moja. Wastani, mashindano ya Caf Yanga ilifanya vizuri kuliko Simba. Ligi Kuu Bara, Yanga na Simba zina wastani sawa wa matokeo. Kinachoifanya Yanga kuwa nyuma ni viporo. Sasa tazama uwekezaji wa Simba, kikosi chake, halafu pima matokeo. Hivi Yanga wamefanya uwekezaji gani mpaka kumtimua Zahera? Utaona kuwa Simba ndio walipaswa kumtimua Aussems kabla ya Yanga kumswaga Zahera. Menejimenti ya Simba ilizubaa sana kufanya uamuzi.

LEVY: Unatetea mauzauza na hili ndo tatizo kuu la Watanzania. Ndo maana ya kukuuliza ni nani kati yao wanaoendesha timu kwa mfumo wa kisasa? Jibu lilitakiwa liwe fupi tu kuwa Yanga wana hulka ya uendeshaji wa kisasa ila hawana uwezo wa kisasa. Na Simba wana kila kitu cha kisasa ila wanaendesha timu kama majiko ya mkaa. Kwa hiyo Yanga ni jiko la gesi Simba ni jiko la mkaa au kuni.

Advertisement