Guinea hiyooo! Yatinga fainali ikiifunga Nigeria penalti 10-9

Wednesday April 24 2019

 

By THOMAS NG'ITU

Timu ya Guinea imefuzu kucheza hatua ya fainali ya Afcon kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 baada ya kuifunga Nigeria kwa mikwaju 10-9.

Timu hizo zilimaliza dakika 90 zikiwa suluhu ya bila kufungana hali iliyowalazimu kwenda hatua ya kupigiana matuta.

 

Hali ilivyokuwa ya mchezo

Katika dakika 45 za kipindi cha kwanza timu zote zilikuwa zikicheza kwa kuviziana huku wakifanya mashambulizi ya kushtukiza kila mmoja.

 Wachezaji wa Nigeria walionekana kutumia nguvu zaidi katika kushambulia huku wakimtumia winga wao Akinkunmi Amoo ambaye alikuwa anatumia spidi kuwapita mabeki wa Guinea. Wakati upande wa Guinea walikuwa wakitumia mipira mirefu kufika kwa mshambuliaji wao Algassime Bah hata hivyo alikuwa anakutana na kigingi kutoka kwa mabeki wa Nigeria waliokuwa wanatumia nguvu na akili.

Advertisement

Nigeria ilifana mabadiliko dakika 45+ kwa kumtoa Akinkunmi Amoo na kuingia Olankule Olusegun ambaye alipoingia alifanya shambulizi baada ya kupiga shuti haa hivyo lilipaa.

Hata hivyo mpaka dakika 45 za kwanza timu hizo zilishindwa kufungana licha ya mara kwa mara kufika langoni kwa mwenzake.

 

Kipindi cha pili kilivyoanza Nigeria walionyesha kuongeza spidi kwenye kushambulia lakini walikuwa wanakutana na kigingi kutoka kwa mabeki wa Guinea. Dakika 55 kiungo wa Nigeria , Fawaz Abdullahi alipiga shuti akiwa katikati ya uwanja na kumchungulia kipa wa Guinea, Sekou Camara hata hivyo mpira ulitoka juu kidogo ya goli.

Guinea walikuwa wanafika mara kwa mara langoni mwa Nigeria lakini umakini wa kuweza kuipita beki ya Nigeria ulikuwa mdogo. Dakika 65 Abah alifanya shambulizi la kushtukiza baada ya kupiga shuti nje ya 18 akitokea upande wa kushoto haa hivyo kipa wa Nigeria, Sunday Stephen aliucheza mpira huo na kuuwahi kuudaka. Katika mchezo huu timu zote zilionyesha ukakamavu lakini washambuliaji wa Nigeria walikuwa wakipata nafasi lakini walishindwa kuzitumia.

 Dakika 61 mshambuliaji wa Nigeria, Wisdom Ubani aliwapiga chenga mabeki wa Nigeria na kupiga shuti kali hata hivyo lilipita pembeni. Dakika 76 Guinea walifanya mabadiliko katika eneo la ushambuliaji baada ya kumtoa Momo Toure na kuingia Mohammed Soumah ili kwenda kuongeza nguvu katika eneo hilo.

 Mabadiliko hayo yalionyesha kuwa na nguvu baada ya Soumah kuonyesha umahiri katika kuumiliki mpira na spidi ambayo ilikuwa inawatesa mabeki wa Nigeria.

Dakika tisini zilimalizika kwa timu hizo kutoka sare 0-0. Katika mchezo huo timu zote zilicheza kwa kukamiana huku kila mmoja akitafuta nafasi ya kushinda lakini umakini ulikuwa mkubwa katika kuzuia.

 Baada ya matokeo ya suluhu dakika 90, Muamuzi Andofetra Rakotojoana kutoka Madagascar, aliamuru kupigwa mikwaju ya penalti ili kupatikana mshindi atakayeenda katika hatua ya fainali. Katika mikwaju ya penalti kulikuwa na kivutio kikubwa baada ya timu zote kuonyesha ufundi katika hatua hiyo.

Guinea walionyesha umahili katika mikwaju ya penalti baada ya kufunga mikwaju yote 10, huku Nigeria wakifunga tisa katika mikwaju 10 baada ya Ogaga Oduko kukosa penalti moja ya mwisho. Wachezaji waliopiga penalti upande wa Guinea, Alya Bangoura, Alya Toure, Aboubacar Conte, Sekou Bangoura, Ahmed Keita, Mahmoud Bangoura, Algassime Bah, Ibrahima Fofana, Ibrahima Dabo na Mohammed Soumah.

Kwa upande wa Nigeria, Ibraheem Jabaar, David Ishaya, Olankule Olusegun, Clement Ikenna, Olatomi Olaniyani,Shedrack Tanko, Fawaz Abdullahi, Wisdom Ubani, Samson Tijani na Ogaga Oduko (alikosa).

 

 

 

Advertisement