Guardiola: Manchester City na Liverpool tunastahili taji la ubingwa

Thursday April 25 2019

 

Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amesema kikosi chake pamoja na kile cha Liverpool wote wanastahili kutwaa taji la ubingwa England baada ya kushinda mechi yao ya jana kwa mabao 2-0 dhidi ya Manchester United.

Kwa ushindi huo wa Manchester City, unaweza kusema kwamba mwenye nyumba ndio karudi unaambiwa na kwa hali ilivyo inawezekana asitoke hata kwenda dukani. Ndio, mabao mawili ya Bernado Silva na Leroy Sane yametosha kuipa alama tatu muhimu Manchester City ya Pep Guardiola. Jana, Guardiola na jeshi lake lilivuka mtaa na kuwafuata wababe wa Old Trafford, Manchester United ya Ole Gunner Solskajer kwenye mchezo wa Ligi Kuu England.
 Kama ilivyotarajiwa na wengi kwamba, Man City ilikuwa inakwenda kupata ushindi kwenye mchezo huo, huku mashabiki wa Man United wakiweka bayana kwamba, haitawauma hata kama watapoteza mchezo huo.
Matokeo hayo yameiweka Man City kileleni ikiwa na alama 89 huku ikifuatiwa na Liverpool wenye pointi 88 na ambao, jana walikuwa wakiishabikia Man United kwa muda ili wawachape wapinzani wao hao kwenye mbio za ubingwa msimu huu. Kipindi cha kwanza, timu zote zilicheza kwa kushambuliana kwa zamu huku Man City wakionekana kumiliki zaidi mpira, lakini hadi mapumziko matokeo yalikuwa sare.
Kipindi cha pili, kiliwachukua Man City dakika tisa kupata bao la kuongoza kupitia kwa Bernado, baada ya shuti lake kumshinda kipa David De Gea.
Bao hilo liliifanya Man United kufunguka kujaribu kupata bao la kusawazisha, lakini wakati wakiendelea kupambana Sane aliyeingia kuchukua nafasi ya Fernandinho, alimaliza shughuli kwa kupachika bao la pili kwa shuti kali akiitendea haki pasi ya Raheem Sterling.
Ushindi huo wa Manchester City umeendelea kutanua rekodi mbovu ya Man United msimu huu, ambapo jana imepoteza mchezo wa sita mfululizo kwenye mechi tisa za karibuni. Pia, umeifanya City kuboresha rekodi zake kwa kufunga bao la 157 kwenye mashindano yote msimu ikivunja rekodi yake yenyewe iliyoiweka msimu wa 2013/14.
Katika mechi nyingine, Arsenal ambao walisafiri hadi kwenye dimba la Molineux kuikabili Wolves, walikutana na kipigo cha aibu kwa kupigwa mabao 3-1. Arsenal imekutana na kipigo hicho ikitoka kuchapwa mabao 3-2 na Crystal Palace kwenye dimba lake la nyumbani, Emirates.
Mabao ya Wolves ambao wamekuwa wababe kwa vigogo wa Top Six msimu huu, yalipachikwa na Ruben Neves, Matt Doherty na Diogo Jota.

Advertisement