Fundi Balama utamu uko hapa!

HABARI ya mjini kwa sasa ni kuhusu Kariakoo Derby itakayopigwa Oktoba 18 kama haitakumbwa na panguapangua ya ratiba ya Ligi Kuu Bara.

Mashabiki wa Simba na Yanga hawawezi kusahau tukio lile la kupindua meza kibabe lililofanywa na Wanajangwani katika mechi yao ya Januari 4, 2020 baada ya kutanguliwa mapema kwa mabao 2-0.

Simba ilitangulia kwa bao la penalti ya dakika ya 42 lililofungwa na Meddie Kagere ‘MK 14’, ambaye alichezwa faulo na Kelvin Yondani.

Kisha mapema katika dakika ya kwanza ya kipindi cha pili, Simba ikapata bao la pili kupitia kwa Mkongomani Deo Kanda, shukrani kwa asisti tamu ya kisigino ya MK 14.

Kutokana na ubora wa kikosi cha mabingwa watetezi Simba, wengi waliamini siku hiyo Yanga ingeoga mvua ya mabao, hasa kutokana na historia ya wachezaji wa Yanga kuingia maji wanapotanguliwa mabao na Simba.

Lakini alikuwa ni Mapinduzi Balama ‘Kipenseli’ aliyeamsha mizuka ya Yanga kupitia bao lake la shuti la mbali kutokea nje ya boksi, baada ya kumnyang’anya mpira Mzamiru Yassin.

Lilikuwa ni bao tamu lililobadili upepo, Yanga ikatawala mchezo hadi kupata bao la pili lililofungwa na Mohammed Issa ‘Banka’ kwa kichwa akimalizia krosi ya Adeyum Saleh.

Bao la Balama si tu liliamsha mzuka wa Yanga, bali pia lilimponza kipa wa Simba, Aishi Manula, ambaye alianza kupigwa benchi baada ya mashabiki kuimba wanamtaka kipa wa pili Beno Kakolanya, wakimtuhumu Manula kufungwa kwa mashuti ya mbali.

Hata hivyo, Manula katika moja ya mahojiano yake, alisema hapaswi kulaumiwa kwa bao lile na kwamba kinachopaswa kufanywa ni kumsifia mfungaji akimvulia kofia Balama kwa roketi lile la masafa marefu.

Na wakati maandalizi ya mechi ya kwanza ya Kariakoo msimu huu yakianza kupamba moto, Kipenseli amezungumza na Mwanaspoti kuhusu maisha yake ya soka.

KWANINI KIPENSELI

Kiungo huyu ambaye kwa sasa ni majeruhi, ameweka wazi sababu za yeye kuitwa kipenseli kuwa ni kutokana na ufupi.

“Hili jina nimepewa na wachezaji wenzangu wa zamani wa Alliance tulipokuwa tunacheza pamoja na kusoma pamoja, waliamua kuniita hivyo kwa madai kuwa mimi ni mfupi kama penseli, ndio limekua hadi sasa siwezi kukataa kwani ni kweli mimi ni mfupi,” anasema.

BABA NA NIDHAMU

Sio kila mzazi anatamani kugundua kipaji cha mwanaye mapema kama ilivyo kwa nchi za wenzetu. Kwa upande wa Watanzania wengi wamekuwa wakiamini katika elimu na kujikuta wakiua vipaji wa watoto wao.

“Haikuwa kazi rahisi kucheza soka kwani baba alikuwa hataki kusikia najihusisha nalo, ni mama pekee ambaye alikuwa anaunga juhudi zangu kwenye mpira,” anasema Mapinduzi na kuongeza:

“Kuna muda nilikuwa natoroka nyumbani kwenda kucheza mpira, lakini kitu kikubwa nilichokuwa nahofia ni kuumia nikiwa uwanjani kwani nilikuwa naogopa nitarudi vipi na nani ataniuguza jambo ambalo lilikuwa linanifanya nicheze kwa nidhamu zaidi.”

Anasema nidhamu hiyo imemsaidia hadi leo katika soka la juu ambapo kufikia sasa ameonyeshwa kadi nyekundu mara moja tu tena akiwa na Yanga kwenye mchezo dhidi ya Pyramids alipobishana na mwamuzi baada ya mchezo.

“Nikiwa Alliance nimecheza mechi zote dakika 90, na sikuwahi kuonyeshwa hata kadi ya njano,” anasema.

“Hata Yanga nimeendeleza nidhamu yangu, nimecheza ligi bila kupata hata kadi ya njano, nafurahia mpira ndio ajira yangu, naahidi kuendeleza ili kumridhisha baba yangu na mashabiki zangu.”

USAJILI BORA

Akizungumzia Yanga ya msimu huu, Balama anasema wana kikosi bora.

“Ni moja ya usajili bora kuwahi kutokea Yanga, wamesajili kutokana na upungufu uliokuwapo, nimefurahishwa na uwezo wa nyota wengi wapya, mashabiki wategemee mambo mazuri waendelee kutupa ushirikiano,” anasema.

“Sina wasiwasi na kipaji changu, sibahatishi, ni mpambanaji, bado naiona nafasi yangu kwenye kikosi cha kwanza, kikubwa natakiwa kuongeza juhudi mazoezini ili niweze kurudi kwenye majukumu yangu ya kawaida na nina imani hilo linawezekana.”

TUKIO LA KUUMIA

Kiungo huo alivunjika mfupa mdogo wa goti akiwa mazoezini baada ya kuangukia mpira akiwa katika harakati za kutaka kuupiga.

“Sikusukumwa na mtu, ni katika harakati zangu za kutaka kupiga mpira niliteleza na kuuangukia kwa mguu tukio ambalo lilinishtua na kuambiwa nimevunjika, haikuwa rahisi kuamini hapohapo hadi maumivu yaliponizidi,” anasema na kuongeza:

“Nilivunjika mfupa mdogo wa mguu wangu wa kushoto na sasa naendelea vizuri, naushukuru uongozi wangu kwa juhudi walizozifanya kuhakikisha natibiwa kwa uangalizi wa hali ya juu, sasa naendelea vizuri.”

NI KIRAKA 2, 7, 10 NA 11

Wakati ukijiuliza jeuri ya Balama katika soka iko wapi hadi anasema nafasi yake kikosini ipo palepale? Lakini pamoja na moto ulionekana kutoka kwa nyota wapya kumbe jamaa anaweza kucheza nafasi nyingi uwanjani.

“Kweli naweza kukosa namba kwenye nafasi zote ninazoweza kucheza namba mbili, saba, kumi na kumi na moja lazima nitapata nafasi tu kwa sababu mpira nauweza.” anasema.

AMPA TANO JAMES BWIRE

James Bwire ni mmiliki wa shule za Alliance ambaye kwa Balama ni mtu muhimu maishani mwake.

Anasema anamshukuru kutokana na kumwamini na kumpa nafasi ambayo imemfanya aonekane anaweza kucheza timu ya taifa sambamba na Yanga.

“Pia nawashukuru wazazi wangu pamoja na kutokuwa na imani na mimi kwenye soka wakitaka nisome lakini baadaye wakaamua kukubali na kuniacha nifanye ninachotaka, na nawashukuru ndugu zangu pamoja na mashabiki kwa kunipa moyo wa kupambana zaidi.”

NA 28 YA BAHATI

Ni lazima mchezaji avae jezi yenye namba mgongoni ikiwa ni moja ya sheria 17 za soka, lakini pamoja na hilo wachezaji wanakuwa na mapenzi na namba kwani kuna wanaovaa kwa kuwa na mapenzi na nyota wa nje, huku wengine wakiwa na maana ya kumbukumbu za tarehe zao za kuzaliwa au miezi.

Kwa upande wa Balama sasa ni bahati.

“Napenda namba 28, ndio jezi yangu ya bahati nimeanza kuitumia tangu zamani na imekuwa na mafanikio kwangu hivyo tu hakuna kitu kingine na kwenye soka naamini kuwa na bahati nayo hadi kufikia hapa nilipo sasa,” anasema.

UCHAWI TUPA KULE

Wakati mastaa wengi wamekuwa wakiamimi katika mazoezi na wengine kuamini ushirikina kwenye soka, Balama anasisitiza kuwa soka ni uwezo na bahati.

“Sijawahi kuamini ushirikina kwenye maisha yangu ya soka, naamini katika uwezo na kujituma mazoezini, uchawi ungekuwa na nafasi nadhani kila kijana angecheza soka kwani angekwenda kuroga tu ili ajipatie riziki, kwangu (ushirikina) hauna maana, kikubwa ni kujituma na kumuweka Mungu mbele kwani ndiye muweza wa yote.”