Fei Toto, Yondani nje Stars

Muktasari:

Nyota 28 wa Taifa Stars wamewasafiri salama nchini Rwanda na wanatarajia kushuka dimbani Jumatatu.

KIUNGO wa Yanga na timu ya Taifa Stars, Feisal Salum 'Fei Toto' amekwama kusafiri na wenzake kuelekea nchini Rwanda kwaajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa kutokana na kukosa hati ya kusafiria.
Wakati Fei Toto akikwama kwenda huko, beki Kelvin Yondani naye hajaondoka kwani anasumbuliwa na majeraha ambapo atakosa mechi hiyo ya kirafiki pamoja na ile ya kufuzu Chan dhidi ya Sudan.
Nyota 28 wamewasili salama mjini Kigali, Rwanda tayari kwaajili ya mchezo huo utakaochezwa Oktoba 14 mwaka huu ambao ni maalumu kujiandaa na mchezo wa kufuzu fainali za Chan dhidi ya Sudan unaotarajiwa kuchezwa Oktoba 18.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa Stars, Etiene Ndayiragije alisema wachezaji wote aliowaita na kufanya nao maandalizi wamesafiri isipokuwa Fei Toto ambaye amekosa hati ya safari.

Alisema nyota wote waliosafiri wameondoka wakiwa katika ari ya mchezo na wanatarajia mchezo mzuri na wa ushindani dhidi ya wapinzani wao Rwanda.
"Wachezaji waliopo wataweza kufiti nafasi ya mchezaji huyo ambaye ameachwa dakika za mwisho nategemea kupata matokeo mazuri kutokana na maandalizi tuliyoyafanya hivyo kilichobaki ni sapoti kutoka kwa watanzania," alisema.
Kwa upande wa Fei Toto alifafanua juu ya hilo kwamba; "Kuna nchi nyingine huwezi kuingia bila pasipoti mpya, halafu nauguliwa na baba yangu ndiyo maana sijasafiri,".