Fei toto atibua usajili Yanga

Muktasari:

  • Kama Fei Toto ataenda kufanya majaribio nchini humo atakuwa ni mchezaji wa pili wa Yanga kwa miaka ya karibuni kufanya hivyo baada ya Mrisho Ngassa kuwahi kwenda West Ham United iliyokuwa chini ya Giafranco Zola, japo alifeli.

KIUNGO wa Yanga Feisal Salum ‘Fei toto anamaliza mwaka wake wa kwanza katika mkataba wa miaka miwili na timu yake, lakini mfukoni ana bonge la dili na kama litakaa sawa hatabakia hapo na hivyo kutibua usajili mzima wa klabu hiyo.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa, Fei Toto anawindwa na klabu moja ya inayocheza Ligi za juu nchini Uingereza na wakati wowote atatimka nchini.

Klabu hiyo ambayo haijawekwa wazi inamtaka kiungo huyo baada ya kuvutiwa na kazi yake, lakini dili hilo litaanzia kwa majaribio kama hatua ya awali.

Endapo kiungo huyo atafuzu majaribio hayo Yanga itaingia mezani na klabu hiyo ambayo bado haijawekwa hadharani.

“Anaweza kuondoka kuna klabu ya England inamtaka, klabu yake inajua lakini bado kuna mambo yanashughulikiwa kwa kuwa kwa sasa kuna hatua ya kwanza inatakiwa kufanyika,” alisema bosi huyo (jina tunalo).

“Feisal anatakiwa kwanza kufanyiwa majaribio akifika kule na kama atafuzu hapo ndipo mambo mengine yatafuata hata mwenyewe anajua.”

Taarifa hizo zikalifanya Mwanaspoti kumtafuta Fei Totoo kujua ukweli wa taarifa hizo lakini mwenyewe alishindwa kukubali au kukataa akijibu kifupi kwa kuuliza:

“Wewe nani kakwambia? Niambie kwanza aliyekwambia hiyo ishu halafu nitakueleza,” alijibu.

Kama Fei Toto ataenda kufanya majaribio nchini humo atakuwa ni mchezaji wa pili wa Yanga kwa miaka ya karibuni kufanya hivyo baada ya Mrisho Ngassa kuwahi kwenda West Ham United iliyokuwa chini ya Giafranco Zola, japo alifeli.

YANGA YASAKA MBADALA

Ndani ya klabu hiyo kujiandaa na hilo inaelezwa mabosi wa klabu hiyo wameanza mipango wa siri kutafuta kiungo mchezeshaji ikitajwa kuwa ni kujiandaa na hali yoyote ya kuondoka kwa Fei Totoo.

“Tumeanza kutafuta kiungo mchezeshaji wa juu ambaye atakuwa na ubora mkubwa tunashirikiana na kocha wetu kuweza kupata mfu mwenye uwezo ambao makocha watahitaji.”

Kiungo huyo alisajiliwa msimu huu kutoka JKU baada ya mabosi wa Yanga kuwazidi maariza wenzao wa Singida United ambao walikuwa wameshamalizana naye kabla ya kutimkia Jangwani na kuonyesha kiwango kilichomfanya aitwe timu ya taifa, Taifa Stars.