Fei Toto ataja mrithi Yanga

Muktasari:

Feisal alipotafutwa jana alizungumza ujio huo wa Makame, akidai Yanga haijakosea kwani huyu ndiye mrithi wake hata akiondoka Jangwani

BAADA ya Meneja wa Feisal Salum kusema hatma ya kiungo huyo itajulikana baada ya kumalizika kwa Fainali za Afcon 2019, mabosi wa Yanga nao wameona wafanye usajili wa maana ili wajiweke fiti kabla halijabaki pengo.
Ndipo fasta wakamdaka, Abdul Aziz Makame ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa Zanzibar Heroes na alikuwa pacha wa Fei Toto aliye injini ya Yanga kwa sasa eneo la kati.
Mwanaspoti linafahamu ukaribu wa wawili hawa tangu wakiwa Ligi Kuu ya Zanzibar na timu ya Taifa ya visiwani na Feisal alipotafutwa jana alizungumza ujio huo wa Makame, akidai Yanga haijakosea kwani huyu ndiye mrithi wake hata akiondoka Jangwani.
“Kama Yanga ikiniruhusu kuondoka naamini kabisa Abdul ni mrithi sahihi kwangu, naamini uwezo wake anapokuwa uwanjani, kuondoka kwangu kutategemea maamuzi ya mabosi wangu kwani bado nina mkataba nao,” alisema.
Fei Toto aliongeza anaamini kabisa kiwango walichokionyesha wakiwa na Zanzibar Heroes watakiendeleza pamoja kama akisalia kikosini Yanga.