Fabiano Joseph amfuata Simbu Olimpiki

Muktasari:

Endapo atafuzu, Fabiano ataungana na Simbu na Failuna Abdi ambao mpaka sasa ndiyo Watanzania waliofuzu kwa michezo hiyo ambayo sasa itaanza Julai 23 hadi Agosti 8 mwakani nchini Japan baada ya mwaka huu kuahirishwa kutokana na janga la corona.

Dar es Salaam. Mwanariadha bingwa wa zamani wa dunia wa mbio za nusu za marathoni, Fabiano Joseph ameanza mazoezi ya marathoni ili kupata muda utakaomuwezesha kufuzu kushiriki Olimpiki 2021.

Fabiano ambaye amekuwa akitamba kimataifa katika mbio za mita  10,000 ambapo alitwaa medali ya shaba ya jumuiya ya madola mwaka 2006 nchini Australia na dhahabu ya nusu marathoni mwaka 2005 nchini Canada amesema ndoto yake sasa ni kushiriki marathoni (km 42) katika Olimpiki.

Kama atafanikiwa kufuzu,  Fabiano ataungana na Alphonce Simbu ambaye tayari amefuzu kushiriki Olimpiki katika marathoni.

Mwanariadha huyo aliyewahi pia kutwaa dhahabu katika mbio za Bogota Half Marathoni na medali mbili za fedha katika mashindano ya dunia ya nusu marathoni na ya dunia ya vijana mwaka 2004 na 2003 ameeleza kuwa ana matarajio makubwa ya kufanya vizuri kwenye marathoni.

"Naamini nimepitia msingi mzuri katika mbio za uwanja ambazo zimenijenga katika kasi na pumzi na huu ni wakati sahihi kwanu kujikita kwenye marathoni, nahitaji kupata muda wa kufuzu Olimpiki lakini pia nishiriki  mashindano ya majeshi, naamini kwa sasa nitafanya vizuri zaidi kwenye marathoni," amesema.

Ingawa Fabiano aliwahi kuchuana katika mbio za marathoni kwa mara ya kwanza kwenye mashindano ya dunia nchini China mwaka 2015 na kumaliza wa 42 na hakuwahi kushiriki tena mbio hizo ndefu za barabarani katika mashindano ya kimataifa tangu wakati huo amesema maandalizi anayoyafanya sasa yamemjenga kiushindani na anatarajia rekodi nzuri si tu kwenye Olimpiki, bali hadi kwenye mashindano ya majeshi mwakani.

"Ninachosubiri ni kalenda ya WA (Shirikisho la Riadha la Dunia), kama mbio za viwango vitafunguliwa mwaka huu, basi nitahakikisha nafuzu Olimpiki mwaka huu na mwakani nitakuwa na programu ya maandalizi ya kwenda kwenye mashindano tu," alisema Fabiano.