Dilunga: Kahata, Ajibu hawanipi presha kabisa Simba

Muktasari:

Dilunga msimu uliopita kocha Patrick Aussems amekuwa akimtumia mara nyingi akitokea benchi

Dar es Salaam. Kiungo wa  Simba, Hassan  Dilunga amesema hana presha kabisa  ya   namba katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo pamoja na ujio wa  Francis Kahata, Sharaf  Shiboub na Ibrahim Ajibu.

Dilunga alisema amejitathimini mapungufu yake ya msimu uliopita hivyo atajitahidi kuyafanyia kazi kipindi hiki cha maandalizi ya msimu ujao ili kuwa bora zaidi.

Kiungo huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar, alisema ataendelea kujituma kwa akili na nguvu zake zote ili kuhakikisha anacheza mara kwa mara kwenye kikosi hicho kama ilivyokuwa msimu uliopita.

“Sina presha kwa sababu najiamini kuwa naweza kupambana kokote na nikapata nafasi ya kucheza, kikubwa mabcho huwa nakitanguliza huwa ni kufuata kile ambacho kocha anataka.

“Msimu uliopita tulikuwa na ushirikiano mzuri, hapakuwa na mchezaji mwenye uhakika wa moja kwa moja kucheza, eneo la kiungo lilikuwa na ushindani, nadhani awamu hii utaendelea,” alisema.

Dilunga alisema itakuwa fahari kwake kuendelea kupata mafanikio na Simba kama ilivyokuwa msimu uliopita ambao walivuka katika makundi na kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Rafiki huyo wa Saimon Msuva, alisema  atakuwa huru kucheza na yeyote kati ya wachezaji wapya ambao watua kwenye kikosi hicho cha wekundu wa Msimbazi.

Simba inajumla ya viungo wanane wa nguvu  ambao mbali ni Dilunga  ni Said Ndemla, Cletous Chama, Jonas Mkude, Francis Kahata, Sharaf  Shiboub, Mzamiru Yassin  na Ibrahim Ajibu.