Dili la Yanga na Ndayiragije mambo yamenoga

Thursday August 6 2020

 

By KHATIMU NAHEKA

KOCHA Mrundi aliyepata mafanikio makubwa ndani ya kipindi kifupi akiwa katika ardhi ya Tanzania, huenda akapewa jukumu la kuiongoza Yanga kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu.

Ni yeye ambaye aliiweka rekodi ya kuichezesha Mbao katika fainali za Kombe la FA kwa msimu wao wa kwanza tu wakiwa Ligi Kuu. Ni yeye pia huyo huyo aliyeng’ara na KMC iliyoshiriki Kombe la Shirikisho katika msimu wao wa kwanza VPL kabla ya kubebwa na Azam FC na baadaye akaibukia Taifa Stars na kuiwezesha kufuzu kwa fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani, Chan.

Na Yanga wanasema kuwa ni yeye wanayemtaka kuchukua mikoba ya Luc Eymael aliyepigwa chini kwa tuhuma za ubaguzi alizotoa akizielekeza kwa mashabiki na uongozi.

Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata ndani ya Yanga jana ni kwamba, hesabu zao asilimia 90 zipo kwa Ettiene Ndayiragije na kocha huyo ameshawajulisha waajiri wake wa sasa, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwa, yuko tayari kutua Yanga kutokana na ofa aliyopewa.

Mabosi wa Yanga wamefanya tathimini ya kina na kukubaliana kwamba, Ndayiragije ni mtu sahihi kwao kufuatia uzoefu wake wa soka la Afrika Mashariki, lakini sio mgeni wa hapa ndani akizifundisha Mbao, KMC na hata Azam FC na ubora wa mbinu zake zinaonekana.

Jina la Ndayiragije linafuta uwezekano wa Kocha Florent Ibenge, ambaye alihitaji muda zaidi kukubali ofa hiyo ya Yanga na Mwanaspoti linafahamu kwamba, ujio wa Rais mpya ndani ya AS Vita, mwanamama Maitre Bestine Kazadi, ambaye ni mtoto wa Rais wa zamani wa klabu hiyo, umempa kiburi Ibenge ambaye pia yuko kwenye rada ya Simba kwa kigezo cha uzoefu wake katika soka la kimataifa.

Advertisement

Uhakika wa Ndayiragije ni kuwa hata wadhamini wa Yanga, GSM nao wamebariki ufundi wa kocha huyo sambamba na bajeti yake kisha mchakato huo kupitishwa na Kamati ya Utendaji ya timu hiyo chini ya Kocha msomi, Dk. Mshindo Msolla.

Habari zinasema Ndayiragije anakuja kukutana na wasaidizi wake wawili pekee raia wa Afrika Kusini, kocha wa viungo Reidoh Berdien na daktari wa viungo Fareed Cassim ambao, wamebakizwa baada ya panga kumkumba Charles Mkwassa, Fred Mbuna, Dk. Shecky Mngazija na Meneja Abeid Mziba.

Pia, Ndayiragije ametakiwa kutafuta kocha msaidizi wake wa kwanza sambamba na kocha wa makipa ambao, wataungana naye kwenye benchi hilo huku lengo kubwa likiwa ni kumuondolea migongano kocha huyo na wasaidizi wake.

“Unajua kwa muda sasa tumekuwa katika malumbano hayo tulikuwa tunamtaka Maxime (Mecky), lakini ni kama ameamua kubaki Kagera Sugar kwa sababu hatupi ushirikiano sana ingawa tumeambiwa ameongeza mkataba kubaki huko ila hatuna uhakika sana kwa kuwa mwenyewe anakanusha,” alisema bosi mmoja mwenye ushawishi ndani ya Yanga.

Habari za ndani ya TFF zinasema kwamba, tayari wameshakubali matokeo ya kumuachia Ndayiragije na mchakato wa siri ndani yao umeanza kutafuta kocha atakayechukua nafasi yake katika kikosi cha Taifa Stars.

Inaelezwa kuwa hatua ya Yanga kumchukua Ndayiragije imeangalia vigezo mbalimbali ikiwemo urahisi wa kuwasiliana kwa lugha tofauti jambo ambalo litarahisisha.

Pia, amekuwa na uzoefu wa kuishi na kufanya kazi na wachezaji wazawa tofauti na makocha wa kigeni ambao, wamekuwa na misuguano mingi. Mbali na Kiswahili, Ndayiragije anajua Kiingereza na Kifaransa.

Hatua hiyo ni kama kwa zawadi kwa mastaa wa timu hiyo wanaokuja kutoka DR Congo akiwemo winga teleza Tuisila Kisinda na Mukoko Tonombe ambao, Mwanaspoti linafahamu kuwa wamemalizana na Yanga na wanasubiri kutua nchini kusaini tu.

Kwa upande wake Ndayiragije alipoulizwa kuhusu dili la kwenda Yanga alisema: “Hata mimi nasikia tu kama wewe, sijajua bado nasubiri.”

Advertisement