Dhamana ya kina Aveva, yasotewa kwa saa nne na nusu

Friday September 20 2019

 

By Imani Makongoro

FAMILIA ya aliyekuwa rais wa Simba, Evance Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange 'Kaburu' sanjari na baadhi ya wadau  wa soka nchini wamesubiri kwa saa nne na nusu kujua hatma ya ndugu zao ambao wanatarajiwa kuwekewa dhamana muda mfupi ujao.
Huku wakiwa na shauku ya kuwaona tena uraiani Aveva na Kaburu, familia na wadau hao walianza kuwasili mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam saa 4 Asubuhi na kukusanyika vikundi vikundi wakisubiri kuanza kwa kesi hiyo ambayo awali ilielezwa kuanza saa 6 Mchana.
Hata hivyo Aveva na Kaburu waliingia kwenye chumba cha mahakama saa. 8:30 sanjari na aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hanspope.
Wakati wakisubiri kesi hiyo kuitwa, wadau hao na wanafamilia walioneka kufarijiana, baadhi wakieleza fursa ya dhamana kwa ndugu zao hao ni jambo la kumshukuru Mungu.
Aveva na Kaburu wamekaa mahabusu siku 814 wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali ikiwamo la utakatishaji fedha ambalo hata hivyo jana Alhamisi mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemkuta na kesi ya kujibu Aveva na wenzake katika makosa manane isipokuwa la utakatishaji fedha.
Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba jana Alhamisi alisema mshitakiwa Aveva na Nyange dhamana ipo wazi hivyo  masharti ya dhamana ni kuwa na wadhamini wawili ambao  watasaini bondi ya Sh 30 Milioni.

Advertisement