Dansa wa Diamond alia ugumu wa maisha

Sunday May 3 2020

 

By Olipa Assa

AHMED Makambi 'Dumy' ni dansa wa mwanamuziki wa kizazi kipya, Diamond Platnum, amesema uwepo wa ugonjwa wa Covid-19 -19 umekwamisha malengo yake ya kuingiza kipato na hivyo maisha kuanza kuwa magumu kutokana na uchumi kuyumba.
Ameliambia Mwanaspoti Online kwa njia ya simu leo Jumapili akiwa nyumbani kwake Mbezi Beach jijini Dar es Salaam kwamba malengo yake ya kwanza ni muziki ambapo kwa sasa hawafanyi ili kuepuka kueneza virusi vya corona.
Lakini malengo ya pili ni kuhusu kituo cha soka kinachoitwa Mabibo Football Foundation kilichoanzishwa mwaka 2018 ambacho kwasasa amesimamisha shughuli ili kupisha janga la corona lipite.
"Hali ni ngumu, kazi zangu zinategemea muziki na kituo cha soka ambacho nina malengo makubwa, tayari nimetengeneza  mawasiliano na watu wa nje kwa ajili ya kuwapeleka wachezaji,'
"Nimewaruhusu vijana kwenda majumbani mwao, nasubiri mpaka hali hii  itakapotengamaa ndipo tuendelee na mchakato mwingine, hali ni ngumu, pesa zinatumika ila haziingii,"amesema.
Dumy ni miongoni mwa madansa wa Diamond Platnum ambao walianza naye kabla hajajulikana, amesema bila shoo anaona kuna changamoto ya mtikisiko wa uchumi.
"Kila mtu yupo nyumbani kwake, akisubiri kwa hamu hili janga lipite, binafsi ninakumbuka shoo ambazo zilikuwa zinatuingizia kipato Ila sina namna ya kufanya zaidi ya kumtazama Mungu atuponye," amesema.

Advertisement