Corona yawapitia mbali mastaa Yanga

Muktasari:

  • Wachezaji wa Yanga wamekutana kufanya vipimo kwa ajili yaaandalizi ya Ligi Kuu Bara ambayo imesimama kutoka na na ugonjwa wa covid 19, ambao unaenezwa na virusi vya corona.

Vipimo vyote vya virusi vya Corona vilivyofanywa na jopo la madaktari wa Yanga leo, vimethibitisha kuwa wachezaji wa timu hiyo hawana maambukizi ya virusi vya corona.

Hilo limefichuliwa na Mwenyekiti wa Yanga, Dk. Mshindo Msolla mara baada ya vipimo hivyo kukamilika leo.

"Wamefanya vipimo vya covid 19, baada ya hapo wakapimwa joto, moyo, uzito na majibu ambayo yametoka kila mchezaji yupo sawa," inasema Msola.

"Baada ya kupata majibu hayo wachezaji wetu wote kuonekana kuwa salama kesho Jumatano saa 10:00 jioni hapa hapa katika uwanja wa shule ya sheria wataanza mazoezi.

" Nimeongea na makocha wote wawili ikiwemo msaidizi, Boniface Mkwasa aliyekuwepo hapa kuwa tayari wamewasiliana na wataanza programu ya mazoezi kama ambavyo walikubaliana," anasema Msolla.

Ukimuondoa kipa Farouk Shikhalo aliyekuwa kwao Kenya, wachezaji wote wa Yanga walikutana leo (Jumanne), kuanzia saa 10:00 jioni katika Shule ya Sheria jijini Dar es Salaam ikiwa ni mikakati ya mwanzo ya kujiandaa na mechi zilizosalia za Ligi Kuu na Kombe la Azam Sports Federation zilizosalia.

Mara baada ya wachezaji hao kukutana wakiwa katika makundi mbalimbali wakizungumza saa 10:30, jioni walianza kikao chao ambacho kilichukua lisaa limoja kikimalizika saa 11:30 jioni.

Mwanaspoti ambalo kilikuwa likifatilia kwa karibu lilibaini baada ya kikao hiko kulikuwepo na madaktari wanne wakitoa maelekezo kwa wachezaji hao juu ya ugonjwa wa covid 19.

Baada ya kumaliza kutoa semina hiyo kwa madaktari hao ambao walizungumzia pia magonjwa mengine wachezaji wote waliokuwepo walifanyiwa vipimo mbalimbali.

Mwenyekiti wa Yanga, Dkt. Mshindo Msola, alieleza kuwa walikuwepo madaktari wanne ambao walitoa semina juu ya ugonjwa wa covid 19, na magonjwa mengine na wachezaji wao waweze kuishi katika mazingira sahihi.