Chilunda, Kelvin waachwa Taifa Stars ikifuata Burundi

Muktasari:

Mshindi kati ya Taifa Stars na Burundi ataingia katika hatua ya makundi ya kusaka kufuzu kwa fainali hizo za Qatar.

Dar es Salaam. Mshambuliaji Shaaban Chilunda, chipukizi Kelvin John ni miongoni mwa wachezaji wanne walioachwa katika kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kilichoondoka nchini leo kuelekea Burundi kwa mchezo wa kutafuta tiketi ya kufuzu mashindano ya Kombe la Dunia yaliyopangwa kufanyika nchini Qatar2022.

Kaimu kocha wa Taifa Stars, Ettiene Ndayiragije ameondoka na wachezaji 21 huku akiwaacha Kelvin John (Serengeti Boys), Baraka Majogoro (Polisi Tanzania), Chilunda (Azam) na Boniface Maganga wa KMC.

Wakati, Chilunda ameachwa kwa sababu ya majeruhi, wachezaji wengine wameachwa kwa sababu mbalimbali. Hata hivyo, wachezaji hao watabaki kambini na kujiunga wenzao mara timu itakaporejea kwa mchezo wa marudiano siku ya Jumapili.

Meneja wa Taifa Stars, Nadir “Cannavaro” Haroub alisema wachezaji wengine wa timu hiyo wapo katika hali nzuri na tayari kupigania taifa lao katika mchezo huo.

“Tumesafiri na wachezaji 21, wanne wapo tayari Burundi tayari kwa mchezo huo. Morali ipo juu na tunatarajia kupata matokeo mazuri hata kama tunacheza uwanja wa ugenini,” alisema Haroub.

Haroub alisema kuwa, wachezaji, Adi Yusuf, Hassan Kessy, Simon Msuva na nahodha, Mbwana Samatta wamekwishawasili Burundi kwa ajili ya mechi hiyo.

Alisema kuwa wamechukua tahadhari kwa ajili ya mchezo huo kwani Burundi ni timu nzuri yenye wachezaji vijana wenye vipaji na wazoefu.

“Ni mechi ngumu kwetu, tunahitaji kuwa makini muda wote, wao watakuwa na mashabiki, sisi watakuwepo pia, lakini siyo wengi,” alisema.

Mshindi kati ya Taifa Stars na Burundi ataingia katika hatua ya makundi ya kusaka kufuzu kwa fainali hizo za Qatar.