Nyoni: Yanga ni bora, lakini inafungika

Muktasari:
- Namungo inatarajia kuwa ugenini dhidi ya Yanga, Mei 13 mwaka huu kwenye Uwanja wa KMC jijini Dar es Salaam ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara.
KIRAKA wa Namungo, Erasto Nyoni amefunguka kuwa hivi sasa wanaitazama zaidi Yanga ambayo ameitaja ni bora lakini inafungika.
Namungo inatarajia kuwa ugenini dhidi ya Yanga, Mei 13 mwaka huu kwenye Uwanja wa KMC jijini Dar es Salaam ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Katika maandalizi ya mchezo huo, Namungo imejichimbia Dodoma huku rekodi zikionesha mara ya mwisho zilipokutana, Yanga ilipata ushindi wa mabao 2-0.
Akizungumza na Mwanaspoti, Nyoni alisema moja ya mipango ya Namungo ni kuhakikisha wanashinda kila mchezo ulio mbele yao ukiwemo dhidi ya Yanga, hivyo wapinzani wao hao wajiandae kwa ushindani mkali.
"Baada ya kuwafunga Mashujaa mwezi uliopita kabla ya ligi kusimama, mikakati yetu ya kujiweka tayari ilianza mapema kwa benchi la ufundi kusawazisha mapungufu na kutupa mbinu imara za kuivaa Yanga ambayo inapambana kutetea taji lao," alisema na kuongeza.
"Tunatambua ubora wao na mapungufu yao, kazi iliyobaki ni kuhakikisha tunafanyia kazi kila tulichoelekezwa kwenye uwanja wa mazoezi ili kufikia malengo ya kukusanya pointi tatu muhimu na kujihakikishia nafasi ya kucheza msimu ujao kama nilivyoeleza mwanzo hatushuki."
Nyoni ambaye amecheza kwa mafanikio Simba kabla ya kutua Namungo, alisema anaifahamu vizuri Yanga na yupo tayari kuipambania Namungo kufikia malengo kwa kuibuka na pointi tatu dhidi ya mabingwa hao watetezi huku akikiri wanakutana na timu bora iliyo sheheni nyota wengi bora na wazoefu.
Namungo ipo nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kucheza mechi 27, imeshinda nane, sare saba na vipigo 12, imefanikiwa kukusanya pointi 31, imebakiza mechi tatu dhidi ya Yanga, Kagera Sugar zote ugenini, kisha itamalizia nyumbani na KenGold.