Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mtihani mgumu mrithi wa Ongala KMC

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula alisema wana imani kubwa na kocha huyo kwa sababu tayari alishawahi kukitumikia kikosi hicho, hivyo watampa ushirikiano wa kutosha kwa mechi zote nne zilizobaki.

BAADA ya KMC kuachana na Kally Ongala, timu hiyo imemrejesha aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Adam Mbwana Mubesh kukiongoza kikosi hicho hadi mwisho wa msimu, huku uongozi ukiweka wazi umempa uhuru wa kufanya kazi bila ya presha.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula alisema wana imani kubwa na kocha huyo kwa sababu tayari alishawahi kukitumikia kikosi hicho, hivyo watampa ushirikiano wa kutosha kwa mechi zote nne zilizobaki.

"Ni kocha anayeijua vizuri KMC kwa sababu alishafanya kazi kabla ya kujiunga na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya kufundisha vijana, tumempa uhuru mkubwa wa kutimiza majukumu yake bila ya presha yoyote," alisema Mwakasungula.

Awali Mubesh aliwahi kufanya kazi Simba kabla ya kujiunga na KMC akiitumikia nafasi ya kocha wa viungo na utimamu wa mwili (Fitness Coach), akiwa na taaluma ya ukocha inayompa fursa kubwa ya kukiongoza kikosi hicho cha Kinondoni.

Kocha huyo alikuwa ni sehemu pia ya benchi la ufundi la timu ya taifa ya Tanzania ya wavulana chini ya umri wa miaka 15, iliyotwaa ubingwa wa Mashindano ya Mabingwa wa Soka Shule za Afrika 2025, yaani African Schools Football Championship huko Ghana.

Kibarua cha kwanza kwa Mubesh kinaanza leo wakati kikosi hicho cha KMC kitakapokuwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar dhidi ya Simba ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Ongala aliyeifundisha pia Azam FC akiwa kocha wa muda na wa washambuliaji, alijiunga na KMC Novemba 14, 2024, akichukua nafasi ya Abdihamid Moallin aliyetimkia Yanga.

Moallin hadi anajiuzulu katika kikosi hicho cha Manispaa ya Kinondoni, alikiongoza kwenye mechi 11 za Ligi Kuu Bara kwa msimu huu na alishinda nne, sare miwili na kupoteza mitano, akiiacha nafasi ya saba na pointi zake 14.

Kwa upande wa Ongala ameiongoza katika mechi 15 za Ligi Kuu Bara na alishinda nne, sare nne na kupoteza saba. Kwa jumla, KMC imecheza mechi 26, ikishinda minane, sare sita na kupoteza 12, ikiwa nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi 30.


MTIHANI ALIONAO

KMC inapambana kutuoangukia kwenye hatari ya kushuka daraja kipindi hiki ikiwa na michezo minne dhidi ya Simba nyumbani, kisha itakwenda ugenini kukabiliana na Tabora United, Mashujaa na Pamba Jiji.

Katika mchezo dhidi ya Simba, Kocha Mobesh ana kazi kubwa ya kufanya kwani kikosi hicho hakijawahi kupata ushindi mbele ya wapinzani wao hao mara 13 walizokutana.

Rekodi zinaonyesha mechi hizo 13 ambazo Simba imecheza dhidi ya KMC tangu Desemba 19, 2018 hadi Novemba 6, 2024, sare ni mbili pekee, huku Simba ikishinda 11 na kufunga mabao 30, huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara tisa.

Kwa sasa Simba inapambana kuisogelea zaidi Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi, kwani tofauti yao ni pointi nne, Simba ikiwa na 66 nafasi ya pili, Yanga inazo 70 kileleni.

Ushindi wa mchezo huu utaifanya Simba kubaki nyuma ya Yanga kwa pointi moja pekee, huku KMC nayo pointi tatu zitaifanya timu hiyo kutokuwa kwenye hatari ya kushuka daraja moja kwa moja na zaidi inaweza kuangukia play off kama itateleza mechi zijazo.

Pia kipa wa Simba, Moussa Camara anaisaka clean sheet ya 17 itakayomfanya kubakiza mbili pekee ili kujihakikishia kumaliza kinara mbele ya Djigui Diarra wa Yanga ambaye sasa anazo 14, mechi nne zilizobaki hata akicheza zote bila ya kuruhusu bao atafikisha 18 wakati Camara akiwa na 19.

Kuna jambo lingine kwa Simba, Jean Charles Ahoua anaendelea kupambana kutanua wigo wa mabao akiwa kinara akifunga 15, akimuacha Clement Mzize wa Yanga mwenye 13. Leonel Ateba wa Simba mwenye mabao 12 sawa na Prince Dube wa Yanga, pia kuna ushindani mwingine wa ufungaji.

Akizungumzia mchezo dhidi ya Simba, Mubesh alisema: "Tumejiandaa vizuri katika mchezo dhidi ya Simba, tumepata siku kadhaa za kujiandaa, tumechambua mechi zao na tulipata nafasi ya kuona wanavyocheza.

"Tuna michezo minne, tunakwenda kucheza na Simba kusaka pointi tatu, huu ni mchezo pekee wa nyumbani hivyo tuna kila sababu za kufanya vizuri kwani tunafahamu mechi tatu zijazo tutakuwa ugenini."

Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola, alisema: "Tuna ratiba ngumu lakini tunamshukuru Mungu mechi tatu tumefanya vizuri imebaki moja, tutahakikisha tunapambana kupata matokeo mazuri.

"Mchezaji ambaye majeruhi hadi sasa ni Mzamiru Yassin pekee, waliobaki wote wapo vizuri kwa ajili ya kuipambania Simba.

"Tunatarajia mchezo mgumu, KMC wamekuwa na matokeo mabaya lakini wana timu nzuri, nina imani kabisa hawatakubali kupoteza mchezo huu, hiyo inatoa picha kwamba mchezo utakuwa mgumu ingawa tumejiandaa kufanya vizuri dhidi ya yao."