Chama atuliza presha Simba

Muktasari:

Chama ni miongoni mwa wachezaji muhimu wa Simba na anakumbukwa zaidi na mashabiki wa timu hiyo kutokana na bao lake la ushindi dhidi ya Nkana, uwanja wa Taifa, lililowavusha kuwapeleka hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018/2019.


Kiungo wa Simba SC, Cletous  Chama anatarajiwa kurejea nchini Juni 8 akitokea  kwao Zambia baada ya kukamilika kwa taratibu za kumrejesha nchini zilizofanywa na klabu hiyo.

Chama ni miongoni mwa wachezaji wa kigeni wa Simba waliorejea nchini mwao baada ya ligi kusimama kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona na walishindwa kujiunga na wenzao kwa wakati kutokana na sheria za kufungwa mipaka na kutotoka nje ya nyumba zao ambazo zimewekwa na nchi zao kama hatua za kukabiliana na virusi hivyo.

Awali Chama alitakiwa kuripoti mwanzoni mwa wiki hii pamoja na Francis Kahata lakini mchakato wa kurejea nchini ukagonga mwamba hivyo anatarajiwa kurejea Juni 8 kwa mujibu wa kocha wake, Sven  Vandenbroeck.

"Chama atarudi nchini Juni 8. Tumekuwa na mawasiliano naye ya karibu kuhakikisha anaenda pamoja nasi, baada ya kurejea itabidi aendelee kuwa chini ya uangalizi kabla ya kujumuika na wachezaji wenzake," alisema Vandenbroeck

Hadi sasa ni wachezaji wawili tu wa Simba ambao hawajawasili katika kambi ya timu huyo ambao ni huyo Chama anayetarajiwa kutua  Juni 8 na Sharaf Shiboub ambaye haijulikani lini atarejea kutokana na marufuku iliyopo nchini kwao Sudan ya kutotoka nje na kufungwa kwa mipaka..

Kuhusu maandalizi ya kuelekea mchezo dhidi ya Ruvu Shooting, Vandenbroeck, alisema yanaendelea vizuri na leo alitoa nafasi kwa wachezaji wake kufanya mazoezi mepesi ili kupumzisha miili yao kutokana na mazoezi ya nguvu ambayo waliyafanya ndani ya wiki.

"Siwezi kusema kuwa wachezaji wangu watakuwa fiti kwa asilimia zote katika mchezo ujao kwa sababu tulikaa muda mrefu bila ya kuwa pamoja na hata kucheza mchezo wowote wa ushindani. Kikawaida inaweza kutuchukua wiki sita kuwa katika kiwango chetu," alisema Vandebroeck

Katika kipindi hiki cha maandalizi kuelekea mchezo wao wa kwanza wa  Ligi, Vandenbroeck alisema wanaweza kuwa na michezo ya kirafiki ili kujiweka fiti. Kabla ya kusitishwa kwa Ligi kutokana na janga la virusi vya corona, Simba ndio waliokuwa wakiongoza msimamo wa Ligi hiyo wakiwa na pointi 71