COSAFA ni bab’kubwa

Tuesday August 13 2019

 

By Charles Abel

HIVI karibuni kutafanyika mkutano wa kimataifa wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambao utafanyika hapa nchini.

Kwenye soka, kundi kubwa la nchi wanachama wa SADC ni wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (COSAFA) isipokuwa Tanzania na DR Congo tu.

Tanzania ni mwanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) wakati DR Congo ni mwanachama wa Shirikisho la Vyama vya soka Afrika ya Kati (UNIFFAC).

Wakati ikionekana kunufaika kuwepo kwenye SADC, upande wa soka mambo bado hayajawa mazuri kwa nchi wanachama wa CECAFA tofauti na ilivyo kwa upande wa COSAFA ambayo inaundwa na nchi zote zilizo Kusini mwa Afrika.

Pengine Tanzania ingeweza kuwa miongoni mwa timu zinazofanya vyema kwenye soka ikiwa ingekuwa miongoni mwa nchi wanachama wa COSAFA badala ya CECAFA.

Licha ya kuwa na umri mrefu, CECAFA inaonekana imeshindwa kutamba vyema kwenye soka barani Afrika kulinganisha na kanda nyingine mfano COSAFA ambayo iko jirani nayo.

Advertisement

COSAFA ilianzishwa mwaka 1997 lakini imepiga hatua kubwa kuliko CECAFA ambayo ni kongwe ikianzishwa mwaka 1927.

Makala hii inajaribu kuonyesha ni kwa jinsi gani CECAFA imeachwa mbali na COSAFA ambayo haina umri mrefu.

Mafanikio kimataifa

Ikiwa na miaka 20 tu tangu ilipoanzishwa, COSAFA imefanikiwa kuwa na uwakilishi kwenye mashindano makubwa ya soka duniani mfano, Fainali za Kombe la Dunia kupitia Afrika Kusini iliyoshiriki mara tatu na Angola iliyoshiriki mara moja.

Sio tu kushiriki bali pia COSAFA imeweza kuandaa Fainali za Kombe la Dunia ambazo zilikuwa za mwaka 2010 zilizofanyika Afrika Kusini jambo ambalo CECAFA haijawahi kufanya wala timu yake kushiriki.

Mfano mwingine ni wanachama wake kutwaa ubingwa wa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mara moja ambapo Zambia walifanya hivyo mwaka 2012.

Uwingi wa mashindano

Ukanda wa COSAFA una idadi kubwa ya mashindano yenye muendelezo mzuri kuliko CECAFA ambayo licha ya ukongwe wake, una mashindano machache ambayo hayana muendelezo.

COSAFA inasimamia na kuendesha mashindano sita tofauti kila mwaka ambayo ni Cosafa Cup kwa wanaume, Mashindano ya Cosafa kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 na yale chini ya miaka 17, mashindano ya wakubwa kwa wanawake, mashindano ya wanawake chini ya umri wa miaka 20 na mashindano ya soka la ufukweni.

Kwa upande wa CECAFA, yenyewe ina mashindano mawili tu ambayo ni yale ya klabu pamoja na Chalenji kwa timu za Taifa ambayo hata hivyo yamekuwa hayana muendelezo na yanafanyika kwa kusuasua.

Idadi ya wadhamini/washirika

Tofauti na CECAFA ambayo imekuwa ikitegemea ufadhili/udhamini wa fedha kutoka kwa Rais wa Rwanda, Paul Kagame na zile za udhamini wa muda mfupi, COSAFA yenyewe ina wadhamini/washiriki wa uhakika ambao wamekuwa wakiihakikishia fedha za kutosha.

Wadhamini wa COSAFA ni Manispaa ya Nelson Mandela Bay, Hollywood Bets, Tsogo Sun, National Lotteries Commission, Supersport na Sasol.

Mastaa wa soka

Ni Mbwana Samatta, MacDonald Mariga na Victor Wanyama ambao wanaweza kuwa mastaa waliotamba kwenye soka duniani wakitokea ukanda wa CECAFA.

Hata hivyo upande wa COSAFA kuna kundi kubwa la mastaa ambao wametamba duniani kama vile Sibusiso Zuma, Shaun Bartlet, Collins Mbesuma, Benni McCarthy na Steven Pienaar.

Advertisement