Bocco, Kapombe watoa tamko

Muktasari:

Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema amefurahia kurejea kwa wachezaji wake na kuhusu aina ya mazoezi waliyofanya kwa mara ya kwanza ni mazuri kulingana na kila walichokuwa wanahitaji kulingana na makosa ambayo wameyafanya katika mchezo uliopita wameyafanyia kazi.

HUKO Msimbazi unaambiwa mzuka umepanda kama wote, baada ya nahodha John Bocco na beki kiraka, Shomary Kapombe kurejea kikosini na jana kutoa kauli kabla ya mchezo wao wa kesho Jumapili dhidi ya Mbeya City.

Simba jana asubuhi walifanya mazoezi kwenye viwanja vya Gymkhana kuanzia saa 4:00-5:30, huku nyota hao wa kikosi cha kwanza wakirejea baada ya kukosekana kwa muda mrefu.Bocco aliumia katika mechi ya ngao ya hisani dhidi ya Azam, huku Kapombe alikuwa akisumbuliwa na maralia.

Katika mazoezi hayo Bocco ambaye awali alikuwa akifanya peke yake pembeni ya uwanja na Kapombe aliyeshindwa kufanya mazoezi na wenzake wote walifanya na wachezaji wanzao tena mazoezi ya nguvu na yale ya aina mbalimbali ya kucheza.

Mwanaspoti ambalo liliweka kambi uwanjani hapo lilimshuhudia Bocco kama bado hajawa fiti kuliamsha dude katika mechi ya kesho kama ilivyo kwa Kapombe.

Mwanaspoti lilizungumza na wachezaji wote wawili na Bocco alisema;

“Kwa sasa naendelea vizuri tofauti na nilivyokuwa mwanzo wakati nimepata haya majeraha na kuhusu suala la kucheza mechi inayofuata hilo si langu bali lipo chini ya makocha wetu,” alisema na kuongeza.

“Kwa sasa naona bado sijafikia katika hali ya kushindana katika mechi ngumu, lakini kwa maendeleo niliyonayo yananipa moyo, sidhani kama naweza kuchukua muda mrefu na kuanza kucheza.”

Kuhusu safu ya ushambuliaji iliyoanza kuwasha moto kabla ya kutulizwa na Mwadui katikati ya wiki hii, Bocco alisema kila anayepata nafasi ya kucheza anaonyesha mchango wake na hata kwa upande wake akipata nafasi hiyo atafanya hivyo kama wengine.

Kwa upande wa Kapombe alisema maendeleo yake ni mazuri tofauti na alivyokuwa mwanzo wakati ameanza kuumwa ndio maana ameweza kufanya mazoezi ya nguvu yote ambayo walifanya pamoja na yale ya kucheza kama wachezaji wengine.

“Nina uwezo wa kucheza kwani nipo fiti ndio maana hata makocha wamenijumuisha kwenye orodha ya wachezaji watakaoingia kambini leo (jana) jioni kwa ajili ya mechi ya Jumapili,” alisema.

“Kuhusu ushindani wa namba, hasa upande wangu wa beki ya kulia, ni kubwa, lakini nilitamani iwe ivyo kwani yoyote ambaye atapata nafasi ya kucheza ataonyesha uwezo wake.”

“Nafurahishwa na uwezo wa juu ambao Haruna Shamte, ambao amekuwa akionyeshwa kwa muda wote ambao nimekuwa nikikosekana katika timu na ushindani unatakiwa kuwepo kokote hata katika maisha ya kila siku,” alisema Kapombe.

MSIKIE AUSSEMS

Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema amefurahia kurejea kwa wachezaji wake na kuhusu aina ya mazoezi waliyofanya kwa mara ya kwanza ni mazuri kulingana na kila walichokuwa wanahitaji kulingana na makosa ambayo wameyafanya katika mchezo uliopita wameyafanyia kazi.

Alisema kuna mazoezi ya kukaba hasa kwa walinzi wake wanne ambayo walifanya yamesababishwa na kufanya baadhi ya makosa ambayo wapinzani wamekuwa wakipenyeza mpira ambayo kwao inawagharimu na wameliona hilo tangu mechi ya kwanza.

“Tukiimarika katika kuzuia makosa hayo ambayo huwa yanawapa mianya wapinzani nadhani kutakuwa tumepunguza mipira mingi hatarishi, lakini nilikuwa nikimtumia Erasto Nyoni na Tairone Santos katika eneo la walinzi wa kati kutokana Pascal Wawa alikuwa na matatizo ambayo yalimfanya haya Shinyanga kutokwenda,” alisema.