Bocco: Azam ni timu nzuri ila Simba SC itaondoka pointi tatu leo na kujikita kileleni Ligi Kuu Tanzania Bara

Muktasari:

Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 12 baada ya kushinda michezo minne itaikabili Azam iliyo nafasi ya nne kwa pointi tisa katika mchezo utakaoanza saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Nahodha wa Simba, John Bocco 'Adebayor' amekiri mchezo wao wa leo jioni dhidi ya Azam utakuwa wa aina yake huku akiweka wazi lengo lao ni ushindi.

Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 12 baada ya kushinda michezo minne itaikabili Azam iliyo nafasi ya nne kwa pointi tisa katika mchezo utakaoanza saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Bocco ameanza mazoezi baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu akisumbuliwa na maumivu ya goti amekili Azam watawapa ushindani mkubwa ila wao watapambana ili kupata ushindi.

"Tunamaini Azam ni timu nzuri ina wachezaji wazoefu na chipukizi kwa hiyo watatupa upinzani mkubwa, lakini tumejipanga kuchukua pointi tatu dhidi yao.

"Timu nzuri zinapambana hivyo mchezo utakuwa mzuri, wenye ushindani na utakaovutia kwani hata aina ya tunavyocheza inaenda kutokana na makocha anaozifundisha timu hii, hivyo mashabiki watarajie upinzani mzuri," alisema Bocco.

Bocco alisema mchezo huo ni muhimu kwetu kwani tunazitaka pointi tatu ili tuzidi kuendelea kuwa kileleni kwenye msimamo wa ligi.

Beki wa Simba, Mbrazil, Gerson Fraga alisema kutokana na mazoezi waliyofanya naamini watashinda mchezo huo.

"Azam ni timu nzuri lakini najua tutawafunga kwani tumefanya mazoezi ya uhakika na binafsi nina hamu ya kukabiliana nao," amesema Fraga.

Kipa Beno Kakolanya alisema licha ya kucheza na Azam katika Ngao ya Jamii mwaka huu na kuwafunga, lakini hakuondoi ubora wa wapinzani wao hivyo leo wataongeza juhudi ili waweze kupata matokeo mazuri.