Biashara yapata pointi moja, kocha atishia kuachia ngazi

Muktasari:

  • Mchezo huu ni wa tatu kwa kila timu huku hakuna ambaye ameonja ladha ya ushindi katika mitanage hiyo.

LICHA ya kuanza kwa kasi mchezo wa leo Ijumaa na kujipatia bao la mapema kupitia straika wao Jeryson Tegete dakika ya saba , Alliance wameshindwa kuondoka na ushindi katika mtanange baada ya kulazimisha sare ya bao 1-1 na Biashara United.
Wakati timu hizo zikitoka sare ya bao hilo, kocha wa Biashara United, Amri Said 'Stam' amesema kikosi chake kinakabiliwa na changamoto ya ukata ambapo wachezaji wake hawajalipwa hadi sasa na kama changamoto hiyo ikiendelea basi anaweza kujiweka pembeni.
Baada ya Alliance kuanza kutikisa nyavu za wapinzani wao, Biashara walitulia na kuanza kutengeneza mashambulizi ambapo dakika ya 40 walisawazisha kupitia Innocent Edwine ambapo lilidumu mpaka dakika zote 90 .
Wakizungumza mara baada ya mechi hiyo,  Stam amesema pointi moja waliyopata sio haba kwani mchezo ulikuwa mgumu hivyo imewapa nguvu kuelekea mchezo ujao dhidi ya JKT Tanzania kabla ya kuwakabili Simba.
"Ni kweli kuna matatizo kwenye timu yetu, wachezaji bado hawajapewa stahiki zao, mimi kama Kocha nitatimiza majukumu yangu lakini changamoto zikiendelea naweza kujiweka pembeni ili kutunza heshima yangu" amesema Stam.
Kocha msaidizi  wa Alliance, Habibu Kondo amesema hawezi kuyataja mapungufu ya wachezaji wake kwa sasa kwani wapinzani wake wanaweza kuyatumia kuwafunga mchezo ujao ila ameahidi kuyafanyia kazi kabla ya mchezo ujao.
Baada ya matokeo hayo, Alliance wamejikusanyia jumla ya pointi mbili katika michezo mitatu waliyocheza huku Biashara United wakipata alama moja pekee katika mitanange mitatu ya Ligi Kuu.