Biashara yaichapa Polisi Tanzania kwao

Sunday October 25 2020
polisi tz pic

KIKOSI cha Biashara Utd kinachonolewa na Francis Baraza kimeshinda 1-0 ugenini dhidi ya Polisi Tanzania mchezo uliopigwa saa 8:00 mchana katika uwanja wa Sheikh Abeid Karume.

Katika mchezo huo timu zote zilikuwa zinacheza kwa umakini huku kila mmoja akisaka bao la kuongoza mapema lakini umakini kwenye safu ya ulinzi katika kila timu ilionekana kutulia.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza hakukuwa na timu yoyote ambayo iliona lango la mwenzake mpaka mpira unaenda mapumziko.

Kipindi cha pili kilianza kwa kushambuliana wakitafuta bao la kuongoza, dakika 52 Biashara Utd walipata bao kupitia kwa Deogratius Judika aliyefyatuka shuti kali na kwenda moja kwa moja wavuni.

Goli hilo halikuonyesha kuwakatisha tamaa kwani safu ya ushambuliaji ya Polisi Tanzania iliyokuwa inaongozwa na Tariq Seif walionekana kuhaha kusaka bao la kusawazisha.

Dakika 67 winga wa Polisi Tanzania, Rashid Juma kidogo aifungie bao la kusawazisha timu yake baada ya kufyatuka shuti kali lakini liliishia mikononi mwa kipa.

Ushindi huo unawafanya Biashara kufikisha pointi 15 na kutoka nafasi ya nne wakisogea mpaka nafasi ya tatu.

Advertisement